Monday, December 23, 2024
Home > Counties > Elgeyo Marakwet > Yahofiwa familia 57 huenda zikakumbwa na maporomoko ya ardhi huko Keiyo

Yahofiwa familia 57 huenda zikakumbwa na maporomoko ya ardhi huko Keiyo

Familia 57 katika eneo la Kapseigut katika kaunti ndogo ya Keiyo Kusini ambazo zimekabiliwa na hatari ya kukumbwa na maporomoko ya ardhi zimetakiwa kuhama mara moja.

Mkuu wa kaunti ya Elgeyo Marakwet, Dkt. Ahmed Omar ameziomba familia hizo kuhamia kwa jamaa zao angalau kwa muda ili kuepuka janga kama lile la huko Pokot Magharibi baada ya nyufa kuonekana katika eneo hilo.

Akizungumza alipozuru eneo hilo mnamo Jumatatu, Dkt. Omar alisema serikali inapanga mikakati ya kuzitafutia familia hizo suluhu la kudumu lakini akasema jambo hili litachukua muda, hivyo basi alizitaka familia hizo ziondoke mahali hapo hadi pale mvua kubwa inayoshuhudiwa kwa sasa itakapopungua.

Pia, aliwataka viongozi katika eneo hilo kutoa orodha ya majina ya familia hizo bila udanganyifu wo wote na pia ripoti ya jiolojia ya eneo hilo kwa afisi yake.

Kwa mujibu wa wakazi wa eneo hilo, walitakiwa kuhama tangu mwaka wa 2013 ambapo ufa ulijitokeza huku ripoti ya jiolojia ikisema kwamba hawafai kuishi katika eneo hilo kwani linaweza kushuhudia maporomoko ya ardhi.

David Kimengich ambaye ni mkazi alisema kwamba waliendelea kuishi licha ya onyo hilo kwa sababu hawana mahali pengine pa kwenda.

Aliongeza kwamba mnamo mwaka wa 2017, ufa huo uliongezeka na hata barabara ya kuelekea Kapseigut kukatika. Aliendelea kusema kwamba nyufa zimeendelea kuongezeka jambo ambalo limewatia hofu.

Waziri wa mazingira katika kaunti hiyo Abraham Barsosio alisikitika kwamba juhudi za viongozi za kuwataka wakazi hao kuhama hazijafua dafu, huku akisema kwamba kuna wakati walilazimika kuwatumia viongozi wa dini lakini hawakufaulu.

Barsosio amewataka wakazi kutilia maanani ushawishi wa serikali na ripoti ya jiolojia ili kuyaokoa maisha yao.

Pia amewasihi wakazi kuacha kuendesha shughuli za ukulima katika sehemu za miinuko kwani hii ndio sababu kuu ya maporomoko ya ardhi.

Hali kadhalika amelitaka bunge la kitaifa kuidhinisha kukatwa kwa sehemu ya msitu wa Kaptagat ili kuwapa makazi watakaohamishwa huku maeneo watakayoacha yakipandwa miti.

Na  Alice  Wanjiru

Leave a Reply