Monday, December 23, 2024
Home > Counties > Wito umetolewa kwa vijana kuepukana na uchochezi

Wito umetolewa kwa vijana kuepukana na uchochezi

Vijana katika kaunti ndogo ya Marakwet Magharibi wamehimizwa kupuuza  wanasiasa wanaoeneza siasa za chuki na matusi  ambazo zinaweza kuleta machafuko.

Naibu kamishna Marakwet Magharibi Bw . Mathias Chishambo alitoa ushauri huo alipokuwa akizungumza kwenye mkutano wa washikadau kuhusu maandalizi ya uchaguzi uliofanyika  ofisini mwake hii leo.

Kulingana na bwana Chishambo, vijana ndio hutumika zaidi na wanasiasa kujitafutia umaarufu hivyo basi wanaweza kutumiwa vibaya kwa kuwachochea wananchi.

Naibu kamishna huyo alisisitiza haja ya vijana kutotumiwa na wanasiasa kuzua rabsha kwenye mikutano ya wapinzani wao.

“Kama humpendi mwanasiasa mmoja kwa sababu ya sera ama mrengo wake wa kisiasa usihudhurie mkutano wake badala ya kwenda kuzua vurugu,”alihimiza Chishambo.

Kama njia moja ya kulinda usalama na kudumisha amani kuelekea uchaguzi mkuu katika eneo hilo, alisema mwanasiasa yeyote atakayewachochea vijana atachukuliwa hatua kali ya kisheria.

Bwana Chishambo alisema wataimarisha doria haswa wakati wa usiku  ili  kuhakikisha kuwa hakuna  mikutano yoyote ya kisiasa itakayofanywa wakati huu.

“Polisi watakuwa wakishika doria hadi usiku kuhakikisha hamna mikutano ya aina yoyote itakayo endeshwa usiku,” alisisitiza.

Pia alieleza haja ya kuwahimiza wahudumu wa bodaboda kutotumiwa na wanasiasa vibaya akisema wengi wao hutoweka baada ya uchaguzi na kuwaacha wananchi mahasimu.

“Hakuna mwanasiasa huishi akiwa adui ya mwanasiasa mwenzake ila sisi ndio huwachwa kama tumechukiana wenyewe baada ya uchaguzi,” aliongeza.

Hata hivyo, aliwarai wananchi wote kuwa waangalifu na kutompa masikio mwanasiasa yeyote atakayeeneza siasa za chuki na uhasama.

By Murugi Job na Rennish Okong’o

Leave a Reply