Saturday, November 23, 2024
Home > Counties > Bungoma > Wataalam wasisitiza utumiaji wa vyakula vya Asili

Wataalam wasisitiza utumiaji wa vyakula vya Asili

Bungoma ni kaunti yenye ukwasi mkubwa wa kuwa na udongo wenye rutuba inayostawisha mimea kama wimbi,mahindi,viazi,njugu,maharagwe na miwa .

Vyakula hivi ni lishe nzuri lakini vimeanza kutoweka kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya hali ya anga,teknolojia na vijana kususia kilimo na kuhamia mijini kutafuta ajira jambo linalosababisha vyakula hivi kuwa nadra kupatikana.

Watu wanaoishi mijini wengi wao hawatumii vyakula vya asili na badala yake wanakula vyakula vilivyotengenezwa viwandani na hivyo kuhatarisha afya zao na kuufanya mwili kudhoofika na hata kukosa nguvu mwilini.

Kulingana na mtaalamu wa tiba ya asili katika kaunti ya Bungoma, Daktari Michael Isaac Misiko, vyakula vinavyoletwa kutoka nje baadhi huwa na madhara kwa afya kutokana na kemikali zinazotumika kuhifadhia vyakula hivyo.

Faida ya vyakula vya asili ni muhimu kwa kujenga nguvu mwilini ndiyo sababu wazee wa kale waliishi miaka mingi bila ya kutosumbuliwa na maradhi ya kila mara na pia walikuwa na afya nzuri.

Kwa mfano chakula kama muwa una upekee wake kwani una uwezo wa kuongeza maji mwilini.Virutubisho vilivyopo katika muwa vina manufaa makubwa katika kusaidia utendaji kazi wa viungo mwilini kama figo,moyo, ubongo na viungo vya uzazi.

Nyakati hizi,watu wengi husumbuliwa na maradhi mengi yakiwemo saratani kutokana na kemikali zinazopatikana katika vyakula vya dukani wanavyovitumia.

Akina mama wa zama hizi, wengi wao wamesahau kupanda mboga za kienyeji, mara mingi utawaona wakienda sokoni ama dukani kununua mboga ambazo zinazalishwa kupitia mfumo mpya kama sukuma wiki hali inayowasababishia wengi wao kukumbana na magonjwa kutokana na kemikali zinazopatikana katika mboga hizo.

Vyakula visivyokuwa vya asili gharama yake ni kubwa mno. Wengi hukimbilia vyakula hivyo kwa mfano mayai kutokana na ukubwa wake pasi na kujali ubora wake.

Vyakula vya asili ni kinga kwa mtumiaji dhidi ya magonjwa mbalimbali ikiwemo saratani ambayo sasa ni tishio kote duniani.

Daktari Misiko alielezea kuwa mojawapo ya njia ya kuboresha afya hata kuongeza wastani wa umri wa kuishi ni pamoja na lishe bora.

Lishe bora hutokana na vyakula bora vinavyozalishwa na kuhifadhiwa katika mazingira salama, alisema.

Mtaalam huyo aliwahimiza watu kukumbatia utumiaji wa vyakula vya asili pakubwa kama njia ya kuongeza kinga mwilini ili kuepukana na magonjwa yanayoweza kutokea kila mara.

Na  Laura Nekesa

Leave a Reply