Zaidi ya wasichana 500 kutoka familia maskini viungani mwa mji wa Narok hapo jana walinufaika na taulo za hedhi zilizotolewa na wanachama wa Muungano wa Amani katika kaunti ya Narok (Narok County Peace Association).
Aidha, wasichana hao pia walipatiwa ushauri nasaha na vilevile kufunzwa hatari inayotokana na dhuluma mbali mbali za kijinsia wanazopitia kama tohara ya watoto wa kike na jinsi ya kuepukana nazo.
Tatizo la ukosefu wa taulo za hedhi au sodo miongoni mwa wasichana hasa wale kutoka familia maskini katika baadhi ya maeneo humu nchini, hasa wakati huu wa janga la Korona ambapo wanfunzi wengi wako nyumbani ni mojawapo ya changamoto zinazowakumba wasichana wengi.
Katika kaunti ya Narok hali hii imepelekea wanachama wa muungano wa amani katika kaunti hii wakiongozwa na balozi wao Bwana Joshua Ole Kaputa pamoja na mwenyekiti wa muungano huo Bi Grace Saningo kutoa msaada wa sodo hizo kwa zaidi ya wasichana 500 kutoka mitaa duni mjini Narok.
Kando na msaada huo wanachama wameungana pia na serikali kujaribu kumaliza dhuluma mbali mbali dhidi ya watoto hao wa kike hasa tohara ya wasichana.
Wakipeana sodo hizo katika uwanja wa michezo wa Ole Ntimama hapo jana, Bi Saningo alisisitiza kwamba wameamua kama wanachama wa amani kuangazia maswala ya watoto wa kike kwani anasema wako katika hatari kubwa na pia huwa wanakumbana na changamoto mbalimbali hasa wakati wao wa hedhi.
Wasichana walionufaika na taulo hizo za hedhi nao hawakuweza kuficha furaha yao.
Wanachama hao walionyesha kutamaushwa kwao na kuongezeka kwa visa vya watoto wasichana kuacha shule katika kaunti hiyo kwa sababu za mimba za mapema, ukeketaji, na ndoa za mapema na kuwaomba washikadau wote kuingilia kati ili kuokoa maisha ya mtoto msichana.
Serikali ya Kenya kupitia kwa idara ya masuala ya jinsia ilizindua mpango wa kuwapa wasichana takriban milioni 3.7 katika shule za msingi, a upili na zile za wanafunzi wenye mahitaji maalum sodo za bure.
Mpango huu ulioanzishwa mwaka wa 2011 umewanufaisha zaidi ya wasichana milioni 11.2 kutoka katika mitaa ya mabanda na sehemu zile zinazoonekana kutengwa. Kufungwa kwa mashule kwa sababu ya janga la Korona ilisimamisha ugawi wa taulo hizi na hivyo kuwawacha wasicha wengi taabani.
Mpango huu ni muhimu kwa vile asilimia 65 ya watu katika nchi hii hawawezi mudu gharama ya sodo.
Ingawa mpango huu una manufaa mengi kwa wasichana wetu,mchango huu wa serikali bado hautoshi na hivyo kuhitaji washikadua wengine kuingilia kati na kuongeza mkono.
By Mabel Keya -Shikuku