Wakurugenzi wawili wa kampuni ya Ken Match East Africa (KMEA) wamezuiliwa korokoroni kwa muda wa siku 10 ili kuruhusu Idara ya Upelelezi kukamilisha uchunguzi dhidi ya madai ya ulaghai wa sukari yenye thamani ya shilingi milioni 16.7.
Jaydeep Rajesh Thanki na Mayur Kumar wanaokabiliwa na shtaka la kupokea mali kupitia kwa njia ya udanganyifu walikamatwa na polisi mnamo tarehe 2 Agosti na tarehe 5 Agosti mwaka huu mtawaliwa.
Hakimu mwandamizi wa korti ya Kiambu, Bi. Patriciah Gichohi awali aliruhusu polisi kuendelea kumzuilia mshukiwa wa kwanza alipofikishwa kortini hapo Jumatatu. Naye mshukiwa wa pili alipofikishwa mbele ya hakimu Bi Stella Atambo, naye pia akawapa polisi kibali cha kumzuilia mshukiwa wa pili Kumar.
Mchunguzi wa kesi, Koplo John Munjama alieleza korti kuwa Rajesh pamoja na Kumar walikuwa wameagiza mifuko 3,980 ya sukari kutoka kaunti ya Mombasa kwa mlalamishi na kuahidi kuwa wangetoa malipo pindi tu wangepokea mizigo hiyo.
Bi. Mary Wangui ambaye ni mlalamishi katika kesi hii naye alipiga ripoti kuwa alikuwa amelaghaiwa sukari yenye thamani ya shilingi milioni 16.7 na washtakiwa ambapo walitiwa mbaroni wakiwa kwenye ofisi za kampuni yao huko Ruaraka.
Walakini, baada ya kupokea sukari walioagiza, Rajesh alimweleza mlalamishi kuwa alikuwa ameweka milioni 4.7 kwenye benki ya DTB jambo ambalo mlalamishi alidhihirisha kuwa halikuwa la ukweli.
Juhudi za mlalamishi kufikia washtakiwa ili aweze kupokezwa malipo ya sukari aliyokuwa amewauzia ziliambulia patupu huku kuzuru kwake katika ofisi zao Ruaraka kukidhihirisha wazi kuwa mali aliyokuwa amepokeza kampuni ya KMEA ilikuwa imemwagika wala isizoleke tena.
Afisa Munjama alieleza Hakimu Mkuu, kuwa walikuwa wamepata habari kuwa washtakiwa walitumia trela tano kusafirisha sukari kutoka bandari ya Mombasa hadi kwenye kampuni yao ya KMEA ambapo wamekuwa wakihudumu kama wakurugenzi wakuu kwa muda mrefu.
Kachero huyu alidokeza kuwa trela hizo zilikuwa zimeonekana nchi jirani ya Uganda na pia washukiwa walikuwa na pasipoti za asili ya taifa la kihindi jambo ambalo liliwapa hofu kwamba iwapo wangeachiliwa kwa dhamana wangetoroka hivyo kuhitilafiana na uchunguzi uliokuwa ukiendelezwa na idara ya upelelezi.
Mahakama ya Kiambu ilimruhusu kachero Munjama kuwazuia washukiwa katika seli za Muthaiga huku polisi wakianzisha msako dhidi ya trela tano ambazo zilitumika kusafirisha sukari hiyo na kubaini jukumu kuu linalotekelezwa na washtakiwa katika kampuni ya KMEA.
Kesi itatajwa tena tarehe 15/8/2019 katika mahakama ya Kiambu.
Na Afwande Pauline/Lydia Shiloya