Huenda waliokuwa madiwani wakati wa serikali za mitaa katika kaunti ya Bungoma waendelee kuteseka kiuchumi iwapo serikali ya sasa ya kaunti haitaingilia kati na kuwapiga jeki kifedha.
Hayo yanajiri ikidaiwa kuwa madiwani hao hawapati msaada kamwe kutoka serikali kuu hali ambayo imewafanya wengi wao kuishi maisha ya ufukara.
Kutokana na mahangaiko hayo sasa wamejitokeza na kuiomba serikali ya kaunti ya Bungoma kuwatetea ili pia wao wapate tabasamu la maisha kama viongozi waliojitolea kikazi eneo hili kabla ya ugatuzi.
Katika mazungumzo na wanahabari, mwenyekiti wa madiwani hao kaunti ya Bungoma, Augustine Tela, alinena kuwa wakati wa hatamu zao walikuwa wakipata malipo duni kinyume na wawakilishi wadi kwa sasa wanaopata mishahara minono pamoja na marupurupu halualua.
Kufuatia hali hiyo, wanasema kuwa mishahara hiyo haikuwawezesha kujiimarisha kimapato.
Bw. Tela alihoji kuwa madiwani hao wakiwa nyumbani kwa sasa wanapitia changamoto si haba za kimaisha kwa kukosa pesa za kukithi mahitaji ya familia zao.
Changamoto hizo ni pamoja na kushindwa kugharamia ada za matibabu,kukosa chakula na pia kushindwa kuwalipia wanawao karo ya shule.
Aidha Bw.Tela alisema sasa wanaomba serikali ya kaunti kupitia Gavana Wycliffe Wangamati kuingilia kati na kuona kuwa maslahi yao yanashughulikiwa kikamilifu.
Hata hivyo akizungumza wakati wa mkutano ulioandaliwa katika eneo la saint Patrick pastoral centre, wadi ya Kabula kwenye eneo bunge la Bumula, uliowaleta pamoja madiwani wa zamani wapatao 265 kutoka maeneo bunge yote ya kaunti, Bw. Wangamati aliwaahidi kuwa tayari mikakati kabambe imewekwa ili kuhakikisha kuwa wanastawishwa kikamilifu.
Aidha Wangamati alitumia fursa hiyo kuwashawishi viongozi hao japo waling’atuka mamlakani kumuunga mkono katika juhudi zake za kuimarisha maendeleo katika kaunti hii.
Na Roseland Lumwamu