Walimu kutoka Kaunti ya Vihiga wamekosoa kauli ya Wizara ya Elimu kutoa amri kwamba wanafunzi wote waliofanya mtihani wa darasa la nane ni sharti wajiunge na shule za upili mwakani.
Wakiongozwa na Katibu wa chama cha kutetea maslahi ya walimu KNUT tawi la Hamisi, Josephat Lubang’a, walimu hao wametaja hatua hiyo kama njia moja ya kusababisha viwango vya masomo nchini kurudi chini.
Akiongea katika hafla ya mazishi ya mwalimu mmoja katika eneo Wadi ya Gisambai, Lubang’a amesema kwamba hatua hiyo itachangia kudidimia kwa viwango vya masomo ikizingatiwa kwamba kuna uhaba wa walimu katika shule nyingi za upili.
Hata hivyo, alishauri kwamba ni vyema serikali izingatie kuajiri walimu wa kutosha nchini kando na kuhakikisha kwamba vifaa vya masomo vimeimarishwa katika shule za upili, kabla ya kuchukua hatua hiyo.
“Tusijidanganye kwamba wanafunzi wote waliofanya mtihani wa darasa la nane walifuzu kujiunga na kidato cha kwanza ndiposa tuamrishe kwamba waingie shule za upili. Tukifanya hivyo hilo litaendelea kuharibu viwango vya masomo katika Taifa letu,” alinena.
Lubang’a alishauri kwamba kile serikali yafaa ifanye ni kutoa nafasi kwa wale watahiniwa ambao hawakufanya vyema katika mitihani hiyo kujiunga na vyuo vya anuwai.
“Kuna vyuo vya masomo ya ufundi kote nchni vyenye vinaendelea kufadhiliwa na serikali ya Kitaifa pamoja na zile za Kaunti. Hivi vyuo vitapata wapi wanafunzi iwapo hatua hii ya Wizara ya Elimu itatiliwa maanani?” aliulizia.
Mwakilishi wadi wa eneo hilo, Eric Odei ambaye alihudhuria hafla hiyo, aliunga mkono matamshi ya walimu hao huku akirai wazazi kuwapeleka watoto wao kwa shule zile ambazo wako na uwezo kulipia karo.
Hata hivyo, alisema kwamba kwa wale ambao hawana uwezo wa kupeleka watoto wao katika shule za upili, nafasi zipo katika vyuo vya ufundi ambako watalipiwa na serikali.
Na Isaiah Nayika