Sunday, December 22, 2024
Home > Counties > Wakaazi wapata afueni baada ya kupata msaada wa chakula

Wakaazi wapata afueni baada ya kupata msaada wa chakula

Wakazi wa maeneo ya Game na Kilo katika Kaunti ndogo la Njoro wamepata afueni baada ya shirika lisilo la kiserikali kuwapa msaada wa chakula, wakati huu ambapo wengi wanakabiliwa na baa la njaa.

Akizungumza wakati wa kupeana chakula hicho, mkurugenzi wa shirika hilo la Serve to Empower Africa, Andrew Muiruri, alisema kuwa hali ya ukame imesababisha hali ngumu ya maisha, hasa ukosefu wa chakula ndiposa kuna umuhimu kwa walioathirika kupata chakula cha msaada kabla ya mvua inayotarajiwa kunyesha.

Kupitia programu zao, shirika hili husaidia familia huko vijijini katika sekta ya elimu, afya ya familia, usafi wa mazingira na mengineyo

Muiruri aliendelea kusema kuwa maeneo haya ni mojawapo ya yale ambayo yanapata mvua ya kutosha lakini kutokana na mabadiliko ya tabianchi, wakazi kwa sasa wanakumbwa na hali ngumu ya kupata lishe.

Wengi wamesukumwa kutumia mbinu ngumu zaidi kutafuta riziki na hivyo basi, Muiruri aliwaomba wasamaria wema kujitokeza zaidi ili kuwaepusha wenyeji na makali zaidi ya njaa kama vile kupoteza wapendwa wao.

Kila familia ilipokea kilo 15 za mahindi katika familia 20 zilizolengwa.

Hivi majuzi, wakati chakula cha msaada kilianza kusambazwa rasmi kupitia serikali ya kaunti ya Nakuru, kamishna wa kaunti hiyo Gilbert Kitiyo alisema kuwa takriban watu 70,000 walio na mapato ya chini wanahitaji chakula.

Alisema kuwa ukosefu wa mvua katika maeneo yaliyoimarika katika kilimo hapo awali, imechangia pakubwa katika ukosefu wa uzalishaji wa chakula cha kutosha.

Na Emily Kadzo 

Leave a Reply