Thursday, December 26, 2024
Home > Counties > Wakaazi waomba suluhu mwafaka kwa shida ya mafuriko

Wakaazi waomba suluhu mwafaka kwa shida ya mafuriko

Wakaazi wa eneo la Kamwaura katika gatuzi dogo la Molo wameiomba serikali kuwasaidia kupata suluhu mwafaka katika barabara ya Njoro-Molo ambapo kumekuwa kukishuhudiwa mafuriko kila wakati mvua inaponyesha.

Semi zao zimesikika siku moja baada ya eneo hilo kupata mafuriko na kusababisha msongamano mkubwa wa magari wakisubiri kukubaliwa kupita na maafisa wa polisi waliokuwa wakipiga doria eneo hilo.

Wakiongozwa na Evans Kinuthia, wakaazi walitoa tetesi kuwa biashara zao huathirika sana msimu wa mvua kutokana na mafuriko eneo hilo na hivyo basi kuomba suluhu ya upesi ili kuwawezesha kuendeleza shughuli zao za kila siku.

“Eneo hili lina wakulima wengi wanaokuza na kusafirisha viazi, kabeji, karoti, mboga aina tofauti na ni vyakula vinavyoharibika kwa upesi. Iwapo hatua haitochukuliwa kwa upesi basi wakulima wataumia,’’ alidokeza Kinuthia.

Aliendelea kusema kuwa sio mara ya kwanza wanashuhudia tukio hili bali ni tukio ambalo linatokea kila msimu wa mvua na sasa wanahitaji ushirikiano ili kupata mwelekeo mwema kuhusiana na jambo hili linalowakera hasa wakulima.

Aliwaomba wazazi kuwasindikiza watoto wao kwenda shuleni kwanzia wiki ijao ambapo muhula wa pili unatarajiwa kuanza ili kupunguza visa vya watoto kuathirika na mafuriko kwa njia moja au nyingine.

“Shule zinafunguliwa wiki ijao na ni ombi langu ya kwamba wazazi watachukua jukumu la kuhakikisha kuwa watoto wao wanaepushwa na athari za mafuriko,’’ alisema Kinuthia.

Hakuna aliyeathirika katika mafuriko yaliyotokea leo kwanzia saa tisa asubuhi. Maafisa wa polisi walichukua hatua ya kufunga barabara hiyo hadi pale mafuriko yalipopungua na kuruhusu magari kuendelea na safari.

Na Emily Kadzo

Leave a Reply