Sunday, December 22, 2024
Home > Environment > Wakaazi walalama kuhusu uchafu na uvundo

Wakaazi walalama kuhusu uchafu na uvundo

Wakazi  wa  mtaa  wa  Cosite mjini Nyahururu, kaunti ya Laikipia, wamelalamikia uchafu na uvundo ulioshamiri katika eneo hilo huku gavana Nderitu Muriithi akiwarai wajitolee kuzoa taka hizo.

Uchafu na  uvundo huu unatokana na mirundiko ya taka kavu kama vile karatasi na maji taka yanayoelekezwa kwenye mto Gathara.

Wakazi  hao waliomtaka gavana wao kuwajibika na kuwasuta wafanyikazi wake, waliudhishwa na majibu ya gavana huyo aliyedai  wajitolee kuzoa taka.

“Usafi unaanza na mtu binafsi, ni jukumu lenu kuhakikisha mnatenga siku maaluum ya kusafisha na kuzoa taka, kasha mniarifu ilinitume wafanyikazi watakaoiondoa kwa gari,” alisema gavana Ndiritu kwenye mkutano na wananchi hao mjini Nyahururu, Ijumaa iliyopita.

“Sisi ni walipa kodi na hatufai kushurutishwa kuzoa taka kwani kuna wafanyikazi wa kaunti waliopewa jukumu hilo.

Uchafu huo una hatari ya kusababisha maradhi kama vile kipindupindu,” alisema Alice Kamau, muuza mboga.

Vile vile walieleza kuwa mifereji ya kuchukulia maji taka iko katika hali mbaya na hivyo kusababisha uvundo katika
mazingira hayo.

“Tunamsihi gavana  atufanyie  ukarabati wa mifereji hii ya kuchukulia maji taka kwani tunalipa kodi kushughulikia hili,” alisema Mwangi Muriuki.

Pia walinung’unika kuhusu idadi chache ya vyoo vya umma, wakisema kuwa kuna choo kimoja tu cha umma kinachowahudumia bila malipo.

Wanjiru Kamau, mchuuzi wa mayai alilalamikia kupigwa marufuku kwa biashara yao, akidai “Maafisa wa afya wanatunyanyasa kwani wanachukua bidhaa zetu za kazi na kuzigawa miongoni mwao.”

Alidai  kuwa imekuwa vigumu kwao kukidhi mahitaji yao, kufuatia marufuku hiyo huku wakimtaka gavana kuwaruhusu kuendelea.

Hata  hivyo, gavana huyo alisema kuwa watatunga sheria zitakazo waongoza wachuuzi katika kazi yao.

Gavana  alisisitiza kuwa vijana katika kaunti hiyo wajiunge na shule za mafunzo ya kiufundi.

Na  Caroline  Muthiani/Rita  Wanjiru

Leave a Reply