Monday, December 23, 2024
Home > Counties > Wakaazi waiomba serikali kuwaletea gari la zima moto 

Wakaazi waiomba serikali kuwaletea gari la zima moto 

Wakaazi wa eneo la Kamwaura, Kuresoi Kaskazini sasa wanaitaka serikali ya kaunti kuwajibika na kuwapa gari la zima moto.

Hii ni baada ya juhudi za kuokoa mali wakati moto unapozuka eneo hilo kufeli hata baada ya kuitisha usaidizi kuuzima moto.

Kulingana nao,  wakaazi wanapoteza mali ya pesa nyingi ikiwemo kisa cha hivi majuzi ambapo mzee mmoja anayefahamika kama Paul Waeri alipoteza mali yake ikiwemo vyumba vinne,  kuku ishirini na tano,  kondoo sita, mbuzi wawili na ng’ombe mmoja waliteketea kwa moto kiasi cha kutojulikana.

Mkaazi, Gitonga Mwangi alisema kuwa visa vya moto vinaendelea kuwa kero kuu kwao na hivyo basi kuiomba serikali ya kaunti kufanya hima kuona kuwa wanapata msaada ufaao wa gari la zima moto pamoja na vifaa vinavyohitajika.

Kwa upande wake, Waeri aliyekuwa bado na mshtuko baada ya kisa hiki, alisema kuwa iwapo wangepata usaidizi kwa wakati ufaao, basi hawangepoteza mali nyingi.

Mkuu wa polisi wa eneo hili, James Atemba alithibitisha kisa hiki na kusema kuwa kulikuwa na moto wa kuni upande wa jikoni wakati Waeri na familia yake walipoenda kulala na kukisiwa kuwa ndio chanzo cha moto huo.

Hata hivyo, Atemba alisema kuwa uchunguzi wa kina umeanzishwa na kuwaomba wakaazi kuwa waangalifu na chochote kile kinachoweza kusababisha moto ili kuepukana na visa kama hivi mbeleni.

Wikendi iliyopita, kulikuwa na mkasa wa moto ambapo nyumba kadhaa eneo la Muthengi ziliungua na hawakuweza kuokoa chochote pia.

na Emily Kadzo/Wesley Njue 

Leave a Reply