Monday, December 23, 2024
Home > Counties > Bungoma > Wakaazi wahimizwa kufuata maagizo ili kudhibiti ugonjwa wa korona

Wakaazi wahimizwa kufuata maagizo ili kudhibiti ugonjwa wa korona

Huku serikali ikiendelea kuweka jitahada za kupambana na janga la korona almaarufu covid-19,wito umetolewa kwa wakaazi wa Bungoma Kusini kuendelea kufuata maagizo yaliyotolewa na Wizara ya Afya ili kudhibiti janga hilo.
Haya ni kwa mujibu wa naibu kamishina wa Bungoma kusini Michael Yator ambaye alisema kuwa janga la korona lipo na hivyo ipo haja wakaazi kuwa makini kwa kufuata taratibu zote ili kushinda vita dhidi ya janga hilo.
Kamishina huyo alitaja kuwa kamati iliyobuniwa ya kushughulikia janga la korona almaarufu Sub-county covid-19 response committee team, inaendelea kuweka mikakati mwafaka ili kuhakikisha kuwa wakaazi wa eneo hilo wanaishi salama dhidi ya korona.
Alisema kuwa kamati hiyo imekuwa ikikabiliwa na changamoto si haba zikiwemo wakaazi kukosa kuvaa barakoa, jambo ambalo anasema iliwalazimu maafisa wa polisi kuingilia kati na kuhakikisha kuwa wale ambao hawajakuwa wakizingatia hayo wanafuata kanuni hiyo ya kuvaa barakoa.
Pia alisema kuwa wengi wa vijana eneo hili wamekuwa na mazoea ya kutangamana kwa makundi wakishiriki katika michezo yao huku akieleza kuwa kamati hiyo imeweza kuweka mikakati ya kuwahamasisha kuzingatia umbali wa hatua ya mita moja unusu.
Alisikitikia jinsi wakaazi wanavyoendeleza shughuli zao bila ya kunawa mikono huku akihoji kuwa huenda hali huyo ikawaweka hatarini ya maambukizi ya virusi vya covid-19 na hivyo kuwataka kuendelea kukumbatia usafi wa kunawa mikono kwa kutumia sabuni au viyeyuzi kama njia ya kudhibiti kuenea kwa virusi vya korona.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari afisini mwake, Yator alisema kuwa serikali ya kitaifa tayari imezisajili familia 7, 537 zisojiweza kutoka eneo la Bungoma Kusini zilizoathirika na janga la korona na mafuriko ili kupata msaada kupitia kijidigitali utakaowasaidia kujikimu kimaisha hususan msimu huu wa korona.
Alitaja kuwa jumla ya familia 200 zilipoteza nyumba zao kutokana na mvua kubwa ambayo imekuwa ikinyesha sehemu nyingi katika eneo hilo, zikiwemo; Kibabii, Mwikubo, Namasanda, Bulondo, East Bukusu, Sio, West, Sang’alo na Namwacha huku akieleza kuwa tayari familia hizo zimewekwa kwenye ratiba hiyo ili kunufaika na msaada huo.
Wakati huo huo Yator alifichua kuwa jumla ya magunia 550 ya chakula, zaidi ya barakoa 5,000 na pia viyeyuzi vimepeanwa kwa familia zisozojiweza kutoka eneo hilo.
Halikadhalika, kiongozi huyo alisema kuwa serikali inaendelea kushirikiana na wakaazi ili kuona kwamba wanasaidika pakubwa kutokana na hali ngumu ya maisha wanayopitia kutokana na athari za covid-19.
Alisema kuwa vijana kutoka vijiji duni kutoka eneo hilo; Bondeni, Wamunyiri, Mjini,Sio, Oldrex, Mandizini, Mteremko na Kamukunji tayari wamesajiliwa na kupewa kazi ya kung’arisha mitaa kama njia ya kuwawezesha kujipatia riziki kupitia kwa mpango wa kazi mtaani.
AidhaYator alihoji kuwa jumla ya watu 124 wa eneo hilo wamepimwa dhidi ya Covid-19 na kati ya idadi hiyo akasema kuwa hakuna aliyepatikana na virusi vya korona na hivyo akawashauri wakaazi wa eneo hilo kuendelea kuzingatia kanuni zote bila kuchoka hadi ugonjwa huo udhibitiwe kikamilifu.
Na Maureen Imbayi

Leave a Reply