Sunday, December 22, 2024
Home > Counties > Waislamu Waombwa Kusaidia Maskini Wakati wa Ramadhan

Waislamu Waombwa Kusaidia Maskini Wakati wa Ramadhan

Waumini wa dini ya Kiislamu Ulimwenguni wamehimizwa kuzingatia shabaha za dini kwa kuwasaidia maskini haswa kwa wakati huu wa mwezi mtukufu wa Ramadhan.

Akizungumza katika hafla ya ugamvi wa vyakula kwa wasiojiweza katika eneo bunge la Mvita, jijini Mombasa, mkereketo wa haki za binadamu Mohammed Salim Mohammed aliwashauri waislamu wote wazingatie nguzo tano za kiislamu haswa kwa kuwasaidia maskini.

Mohammed alisikitika kuwa jinamizi la korona linanokumba Dunia nzima limefanya maisha kuwa magumu na kutishia maisha ya wengi hasa wasiojiweza.

Kwa hivyo aliwahimiza waislamu na waumini wa dini nyenginezo kujaribu kadri wa uwezo kusaidia wasiojikimu.

“Inasikitisha sana kuona jamii maskini na za mitaa wakizidi kuumia njaa na baridi haswa msimu huu wa mvua bila kupata usaidizi,” alisema Mkereketo Mohammed

Mohammed aliwasihi waislamu waonyeshe imani zao kwa vitendo kwani Mwenyezi Mungu atawaongezea kwa kuwajali wasiojiweza.

Alidokeza kwamba mwezi mtukufu wa Ramadhan ni mwezi wa ibada na kutenda mambo mengi ya kheri kwa kusaidia jamii.

Kiongozi huyo alisema alichukua fursa ya mwanzo wa mwezi huu mtukufu kama njia mojawapo ya kuwatakia waislamu wenzake Ramadhan karim.

Alisema pia kuwa alitaka kuwasaidia vibarua ambao hutegemea vibarua vya kila siku ili kujikimu na familia zao

Mohammed aliwashauri waislamu waongeze ibada zaidi wakati huu wa mwezi mtukufu wa Ramadhan na kuwasaidia majirani.

Katika hafla hiyo watu elfu moja ambao hawajiwezi walinufaika na vyakula,vinywaji pamoja na maji ya chupa kutoka kwa kiongozi huyo

Na Joseph Kamolo

Leave a Reply