Friday, November 15, 2024
Home > Counties > Elgeyo Marakwet > Wahudumu wa afya watishia kugoma

Wahudumu wa afya watishia kugoma

Wahudumu wa afya katika kaunti ya Elgeyo Marakwet wameipa serikali kuu na ile ya kaunti makataa ya wiki moja kusawazisha marupurupu yaliyotangazwa na serikali kwao wanapoendelea kupigana na ugonjwa wa corona la sivyo, watagoma.

Katibu mkuu wa chama cha wauguzi katika kaunti, Benson Biwott alisema ingawa wanamshukuru rais kwa kuwatambua kama maafisa wa mstari wa mbele katika vita dhidi ya covid-19, wanahisi kutengwa kulingana na ugawaji wa marupurupu hayo.

Biwott alisema hawaelewi kwa nini madaktari wapate Sh.20,000, huku wafanyi kazi wa chini wakipata Sh.5,000 kila mwezi kwa muda wa miezi mitatu ijayo ilhali wote wanakabiliwa na hatari sawa ya kuambukizwa virusi vya corona.

“Kila mfanyi kazi wa afya kuanzia bawabu anayepokea mgonjwa anapoingia hospitalini, yule anayedumisha usafi katika vituo vya afya na wataalam wote wa afya hata wale wa maabara wamo hatarini ya kuambukizwa ugonjwa huu,” alisema Biwott.

Aliendelea kusema kuwa wahudumu wa afya wamekuwa wakikabiliwa na hatari wanapohudumia wagonjwa akitaja mkurupuko wa homa ya manjano ambapo baadhi yao waliaga dunia na kwa hivyo akaitaka serikali kuwapa bima ya afya itakayowashughulikia.

Katibu wa chama cha maafisa wa kliniki Mark Kipsang aliitaka serikali kuwapa wahudumu wote wa afya mafunzo ya kutosha kuhusu ugonjwa huu wa corona ili wawe wamejihami vilivyo kupigana nao.

“Huu ni ugonjwa mpya ambao hakuna anayeuelewa na kwa hivyo wahudumu wote wanafaa kupewa mafunzo ya kutosha,” alisema Kipsang.

Biwott alisema kufikia sasa, kaunti hiyo haina vifaa vya kutosha vya kujikinga kutokana na ugonjwa huo iwapo kutakuwa na mtu atakayeugua ugonjwa huo.

Hivyo basi aliwashauri wahudumu hao wasihatarishe maisha yao kuwahudumia wagonjwa ambao wana dalili za covid-19 ikiwa hawana vifaa vya kujikinga.

Katibu huyo alisema wanajua huu si wakati mzuri wa kugoma nchi inapokabiliwa na ugonjwa huu ambao umeenea duniani kote lakini hawana budi ikiwa serikali haitatimiza matakwa yao.

Na  Alice Wanjiru

Leave a Reply