Sunday, December 22, 2024
Home > Counties > Bungoma > Wafungwa washiriki uchaguzi Bungoma

Wafungwa washiriki uchaguzi Bungoma

Huku taifa nzima likiwa katika pilikapilika za upigaji kura, wafungwa katika kaunti ya Bungoma hawakuachwa nyuma kwani maafisa wa magereza pamoja na usimamizi wa magereza kaunti hiyo ukiongozwa na mkuu wa magereza Bungoma Aggrey Akoyo alitoa fursa kwa wafungwa hao kushiriki uchaguzi.

Akizungumza na KNA, mkuu huyo wa magereza alieleza kuwa ni haki ya kila mwananchi kushiriki katika uchaguzi kwani maisha ni safari ambayo kesho yake haiwezi kutabiriwa.

Kwa mujibu wa Bw Akoyo, takriban wafungwa 19 walisajiliwa kama wapiga kura katika kituo cha magereza cha Bungoma, ila kutokana na masuala ibuka yasiyohepukika, ni wafungwa kumi na sita pekee ndiyo walioshiriki uchaguzi katika kituo hicho.

“Sio kituo cha magereza cha Bungoma tu ndicho kilichoshiriki uchaguzi ila takriban wafungwa wote katika kaunti yetu ya Bungoma wamepewa nafasi kushiriki katika zoezi hili la kikatiba,” Bw Akoyo alikariri.

Mkuu huyo wa magereza pia aliwapongeza wote waliojitokeza kushiriki katika zoezi hilo na kuwarai wananchi wote kudumisha anmani katika kipindi hiki cha uchaguzi ili kuepuka makabiliano baina yao na polisi pamoja na kuilinda nchi yao.

Kwa mujibu wa Victor Ndiwa ambaye ni mfungwa katika gereza la Bungoma na ambaye pia  alishiriki katika uchaguzi huo, zoezi hilo lilikuwa la huru na la haki kwani hapakuripotiwa visa vyovyote vya ushawishi wa wapiga kura ndani ya gereza hilo.

“Naishikuru serikali pamoja na usimamizi wa magereza katika kaunti yetu ya Bungoma kwa kuturuhusu kushiriki katika zoezi hili muhimu,” Ndiwa alisema.

Na Mwangi Oliver and Roseland Lumwamu

Leave a Reply