Monday, December 23, 2024
Home > Counties > Bungoma > Wafanyakazi wa Juakali wanufaika na barakoa mjini Bungoma

Wafanyakazi wa Juakali wanufaika na barakoa mjini Bungoma

Wafanyakazi wa sekta ya juakali katika kaunti ya Bungoma siku ya Jumamosi walikuwa na kila sababu ya kutabasamu baada ya kupokea barakoa kutoka kwa serikali ya kaunti hiyo kama njia mojawapo ya kudhibiti maambukizi ya korona.
Akizungumza wakati wa kuwakabidhi bidhaa hizo muhimu mjini Bungoma, Gavana Wycliffe Wafula Wangamati alisema kuwa mpango huo ulilenga kuwafaidi zaidi wahudumu wa bodaboda,wachuuzi wa mboga na matunda,wahudumu wa matatu pamoja na wagonjwa wanaotembelea vituo vya afya vya serikali kutafuta matibabu.
“Kwanza tunataka kupeana barakoa hizi Kwa wafanyakazi wa juakali ili wajikinge dhidi ya ugonjwa wa korona,”alisema Wangamati.
Wangamati alidokeza kuwa kuvaa barakoa kutasaidia pakubwa kupunguza kuenea kwa kirusi cha korona.
Aidha alisema kuwa serikali yake inatafuta namna na mikakati ya kutengeneza barakoa ili wakazi wasihangaike kupata bidhaa hizo muhimu.
Hayo yanajiri baada ya waziri wa usalama wa ndani Fred Matiang’i kuwahadharisha wakenya watakaopatikana wakivunja amri ya kuvaa barakoa kuwa watatiwa mbaroni kwa miezi sita au kupigwa faini ya takribani shillingi elfu ishirini (20,000).
Gavana Wangamati alidokeza kuwa kwa sasa kituo maalum cha kuwatenga waathiriwa wa covid-19 katika hospitali ya rufaa ya Webuye kiko tayari kwa ya kuwahudumia wagonjwa hao.
Alisema kuwa serikali ya kaunti hiyo ilianzisha mpango wa kuchukua sampuli za watu walioshukiwa kutangamana na wagonjwa wa covid-19 na kupelekwa kufanyiwa uchunguzi wa kimaabara katika kaunti ya Kisumu na Nairobi huku akihoji kuwa kati ya watu 70 waliofanyiwa uchunguzi huo wote walipatikana salama.
Aidha Bw. Wangamati alieleza kuwa wahudumu wa afya wapatao 300 tayari wamepokea mafunzo kuhusu jinsi ya kuwahudumia wagonjwa wa covid-19.
Tumekuwa tukiwapa mafunzo wahudumu wa afya jinsi ya kukabiliana na covid-19.Tunapoongea sasa,tayari wataalam300 wamefunzwa na tutaendelea kuwafunza madaktari hao,” akadokeza.
Wangamati aidha alitaka kuwepo ushirikiano kati ya wananchi na serikali ili kukabiliana na janga hilo la covid-19.
Bw.Wangamati alikiri kuwa serikali yake imekumbatia ushirikiano na serikali kuu ili kuweka mikakati ya kuwasaidia wananchi kutokana na masaibu wanayopitia wakati huu wa janga la korona.
“Tutaendelea kushirikiana kwa karibu ili kuwasaidia wananchi baadhi ya mikakati mingine kwa kuwapa chakula watu walioathirika na janga hili hatari la korona,” akasema
Gavana Wangamati akihutubia wanajuakali kabla ya kuwapatia barakoa katika juhudi ya kukabiliana na ugonjwa wa Corona.

Na Roseland Lumwamu

2 Attachments

Leave a Reply