Thursday, December 26, 2024
Home > Counties > Waendeshaji bodaboda waombwa kutii sheria za trafiki ili kuzuia maafa barabarani

Waendeshaji bodaboda waombwa kutii sheria za trafiki ili kuzuia maafa barabarani

Kamanda wa polisi katika eneo bunge la Molo, Timon Odingo amewataka waendeshaji bodaboda kuwa waangalifu barabarani na kutii sheria za trafiki kikamilifu kwa minajili ya kupunguza maafa zaidi.

Matamshi yake yanajiri siku moja baada ya mwanamke mmoja wa umri wa makamu kupoteza maisha yake katika eneo la Munju lililoko katika barabara ya Njoro-Molo baada ya pikipiki waliyokuwa wakisafiria pamoja na bintiye kugongwa na lori.

Kwa mujibu wa Odingo, hii ni mojawapo ya ajali ambayo ingeepukika iwapo mwendeshaji bodaboda angeipa lori nafasi kupita kabla ya kuingia barabarani na kuelekea upande mwingine.

Alisema kuwa tukio hili linavunja moyo sana na ni sharti waendeshaji bodaboda kutii sheria za barabarani zikiwemo kwenda kwa mwendo unaostahili, kumpa mwingine nafasi ya kupita bila kubishana, kutotumia vileo wakati wa kuendesha bodaboda, kuvaa mavazi yanayostahili barabarani, kuwaheshimu madereva wengine na hata wapita njia barabarani ili kuleta utaratibu unaostahili barabarani.

Aidha, aliendelea kusema kuwa hawatachoka kuwachukulia hatua za kisheria kwa wale walio na uzoefu wa kutotilia maanani sheria hizi akiongeza kuwa wataendelea kuimarisha doria ili kuhakikisha kuwa wale waendeshaji bodaboda wasiotii sheria za barabarani hawaweki maisha ya wateja wao hatarini.

Odingo anaamini kuwa wengi wa waendeshaji bodaboda wamepitia masomo ya udereva, wamepata mafunzo kadha wa kadha hata kupitia mamlaka ya kitaifa ya usafiri na usalama ya NTSA na hata maafisa wa polisi na hivyo basi hatarajii wakati mgumu katika utendakazi wao nao iwapo watatii sheria.

Mwili wa mwendazake aliyefahamika kama Lydia Muthoni ulipelekwa katika makafani ya hospitali ya gatuzi dogo la Molo huku bintiye Muthoni aliye na umri wa miaka 12 pamoja na mwendeshaji bodaboda walipokea matibabu katika hospitali ii hii na kuruhusiwa kwenda nyumbani.

Emily Kadzo na Joel Angode

Leave a Reply