Sunday, December 22, 2024
Home > Counties > Wabunge wataka ngoma ya BBI isimamishwe

Wabunge wataka ngoma ya BBI isimamishwe

Baadhi ya wabunge wanaoegemea upande wa naibu wa rais William Ruto wametaka mjadala kuhusu ripoti ya BBI kusitishwa kwanza hadi pale janga la Corona ambalo linaendelea kutikisa sio tu taifa hili bali ulimwengu mzima, litakapoweza kukabiliwa.
Wabunge hao wakiongozwa na mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria, Ken Kiloku wa Narok mashariki, Gabriel Ole Tongoyo wa Narok magharibi, mbunge mwakilishi wa kaunti ya Narok Soipan Kudate miongoni mwa viongozi wengine wamesisitiza haja ya maswala mengine ambayo yanaweza kungoja kwanza kusitishwa ili kuokoa maisha ya wakenya wengi ambao wanadai wanaendelea kuangamia kutokana na janga la Corona.
Wakiongea kwenye hafla ya mchango katika kanisa la katoliki katika eneo la Nairegie Enkare katika kaunti ndogo ya Narok mashariki juma hili, wambunge hao walishikilia kwamba swala la BBI sio swala la dharura kwa hivi sasa na serikali inafaa kutafuta namna ya kuwasaidia maafisa wa afya sawa na kuimarisha hali ya hospitali na vituo vya afya humu nchini ili kupambana kabisa na janga hilo.
Vile vile, wabunge hao wamependekeza maoni ya kila mwananchi kutiliwa maanani na kujumuishwa kwenye ripoti hiyo ili iweze kuafikia lengo lake la kupatanisha Wakenya wote.
“Tusikimbilie kura ya maoni, hii BBI ni ya Wakenya wote na ingekuwa vyema kama maoni ya kila mmoja ingejumuishwa.Tukae chini tuviangalie vipengee vyote vinvayoleta utata ili moani ya wote yaweze kujumuishwa,” alisema Kuria.
Bi Soipan naye kwa upande wake alisema atachukua muda wake kusoma ripoti hiyo ili aweze kuwaelemisha wenyeji wa Narok.
“Wafanyikazi wetu wa afya ambao wako mstari wa mbele katika kupigana na janga hii la Corona wanaumia, wanakufa, tuwashughulikie kwanza tuwape vifaa na marupurupu ndiposa tuangalie ripoti ya BBI,” alidokeza Kiloku huku akiongeza kwamba hata maafisa wa usalama wanafanya kazi ngumu wakati huu na wanastahili marupurupu.
Mpango wa BBI ulitokana na maelewano baina ya Rais Uhuru Kenyatta na kinara wa cha cha chungwa (ODM) Bwana Raila Odinga mnamo Mechi 9 mwaka wa 2018 ambapo walikuja pamoja na kusalamiana na kuanzisha mwongozo wa kuileta nchi pamoja baada ya ghasia zilozo zuka nchini baada ya marudio ya uchaguzi ya Oktoba 26 2017 uliosusiwa na upinzani ukiongozwa na bwana Odinga.
Baada ya maelewano hayo, safari ya kuandaa ripoti ya BBI ilianza ambayo inahusisha kubadilisha vipengee kadhaa katika katiba ili kujaribu kuleta mwafaka wa kudumu nchini.
Tume iliyoteuliwa kufanya kazi hii inaongozwa na Seneta wa kaunti ya Garissa Bwana Yusuf Haji ambayo iliadaa ripoti baada ya kukusanya maoni kutoka kwa wananchi kutoka Kenya nzima kisha ripoti hiyo ikawasilishwa kwa Rais na Bwana Odinga na sasa inaelekea kupigiwa kura ya maoni hapo mwakani.
Ripoti hiyo ilijumuisha vipengee tisa vya mwafaka wa maelewano baina ya Rais na Bwana Odinga ikiwemo kupigana na ufisadi, ugatuzi, uhasama wa kijamii wakati wa kura na mambo mengineyo.

By Mabel Keya-Shikuk

 

Leave a Reply