Monday, December 23, 2024
Home > Counties > Usalama waimarishwa kaunti ya Nakuru huku mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne ukiendelea

Usalama waimarishwa kaunti ya Nakuru huku mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne ukiendelea

Kaunti kamishna wa Nakuru, Loyford Kibaara amesema kuwa usalama umeimarishwa katika sehemu ambazo zimekumbwa na utovu wa usalama ili kuhakikisha kuwa watahiniwa wanafanya mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne kwa amani.

Bw. Kibaara alisema kuwa maafisa wa polisi wamearifiwa vema kuhusiana na utekelezaji wa kazi yao wakati wa mitihani itakayochukuwa muda wa mwezi mmoja na hivyo basi wanatarajiwa kuwa macho ili kuzuia visa vya ukosefu wa usalama katika kipindi cha mitihani .

Baadhi ya sehemu ambazo zimekumbwa na utovu wa usalama ni kama vile Rhonda, Kaptembwo, Kivumbini ambapo kumetokea uvamizi wa vijana kutoka magenge haramu ikiwemo ya Confirm, Watizedi na Mauki.

Kadhalika, katika maeneo ya Mariashoni kumekuwa na uhasama wa kikabila kila upande uking’ang’ania rasilmali za misitu huku baadhi ya watu wakishambuliwa kwa mishale, na kuachwa wakiuguza majeraha.

Akizungumza afisini mwake, Bw. Kibaara alidokeza kuwa usalama wa usafirishaji wa mitihani katika vituo tofauti umeimarishwa huku akionya kuwa yeyote atakayepatikana akikiuka sheria za usalama wa mitihani atachukuliwa hatua za kisheria.

Katika kaunti ya Nakuru iliyo na vituo 480 vya mitihani, idadi ya watahiniwa wanaofanya mtihani huu wa kidato cha nne unaoendelea ni 46,086 wakiwemo wavulana 23,075 na wasichana 23,011.

Na Emily Kadzo 

Leave a Reply