Tuesday, November 12, 2024
Home > Counties > Ukulima katika misitu uangaliwe upya

Ukulima katika misitu uangaliwe upya

Mwanachama wa bodi ya shirika la misitu nchini amependekeza kuundwa kwa timu itakayohusisha mashirika mbalimbali kuchunguza changamoto zinazokabili ukulima katika misitu ya serikali.

Joel Ego alisema kwamba mpango huo ulionuia kuimarisha maisha ya watu wanaoishi karibu na misitu kwa kuwakubalia waendeshe shughuli za ukulima katika misitu huku wakichunga miche,mpango ambao  ulipingwa na jopo kazi lililoundwa kuangalia usimamizi wa misitu nchini.

Ego aliyeongoza shughuli za upanzi wa miti katika msitu wa Sing’ore kaunti ya Elgeyo Marakwet alisema  ni muhimu uchunguzi ufanywe ili kujua hasa ni changamoto zipi zinazoukabili mpango huo.

Jopo hilo lilipendekeza kusitishwa kwa mpango huo likisema ulitumiwa vibaya na maafisa wa KFS, wananchi na hata viongozi.

Hata hivyo kulingana na Ego, mpango huo hauna dosari ila wale waliokuwa wanautekeleza  hawakufuata masharti yaliyowekwa na hivyo basi kusababisha kusitishwa kwake na kwa hivyo ni muhimu uangaliwe upya.

Ego pia alisema kwamba marufuku iliyowekwa na serikali dhidi ya ukataji wa miti kutoka misitu ya serikali haijaathiri tu wafanyi biashara bali pia shirika la KFS ambalo linapoteza ushuru wa mamilioni ya pesa.

Alisema kuna miti mingi katika misitu ya serikali ambayo imekomaa na inafaa kuuzwa lakini kutokana na marufuku hiyo hili haliwezekani.

“Miti ni aina ya mimea na kama mimea yoyote ile inafaa kuvunwa inapokomaa lakini hili haliwezekani kutokana na marufuku hiyo,” alisema Ego.

Hata hivyo alisema marufuku hiyo inaweza kuondolewa tu ikiwa shirika hilo litaweka mikakati itakayomridhisha Waziri wa Mazingira na Misitu.

Wakulima na wafanyi biashara wanaoishi karibu na msitu wa Sing’ore walikuwa wameitaka serikali kuangalia suala la marufuku na lile la ukulima wakisema kwamba wengi wanategemea msitu kujikimu kimaisha.

Mwanachama huyo aliyekuwa ameandamana na Kamishina  wa kaunti hiyo  Dkt. Ahmed Omar na kamati ya usalama pia aliwataka Wakenya kupanda miti kwa wingi ili kuhakikisha asilimia 10 ya ardhi nchini iko na misitu kufikia mwaka wa 2022.

Ego pia aliwashauri wakazi wa kaunti hii kupanda miti kwa wingi kuzuia visa vya maporomoko ya ardhi ambayo husababisha vifo na uharibifu wa mali.

Na   Alice Wanjiru

Leave a Reply