Tangazo la Rais Dr William Ruto kuwa atatenga fedha za kutosha kwa ajili ya kuboresha idara ya mahakama limepongezwa na baadhi ya mawakili na wakazi wa kaunti ya Busia.
Kwenye hotuba yake wakati wa hafla ya kuapishwa kwake katika uwanja wa michezo wa Kasarani jijini Nairobi hapo jana, rais Dkt. William Ruto alitangaza kuwa serikali yake itatenga shilingi bilioni tatu kila mwaka kwa idara ya mahakama.
Kando na fedha hizo, rais Ruto aliahidi kushirikiana na Idara ya Mahakama katika kujenga mahakama kuu katika kaunti saba nchini na maakama ndogo katika kaunti ndogo 123 nchini ili kusongesha huduma za mahakama karibu na wananchi.
Hatua hiyo imepongezwa na mawakili kutoka Kaunti ya Busia kupitia mwenyekiti wa chama chao cha LSK Maxwell Okeyo ambaye anasema itasaidia pakubwa katika kuboresha utendakazi wa idara ya mahakama.
“Kaunti ya Busia ni kati ya kaunti ambayo maswala ya mahakama imesalia kwenye mji wa Busia licha ya kuwa na mahakama ndogo Malaba na Funyula. Hii inatokana na ukosefu wa miundo msingi ya kutosha kuisimamia idara hio muhimu,” alisema Okeyo.
Usemi wake umeungwa mkono na baadhi ya wakazi kutoka maeneo ya Teso kaskazini, Budalang’i na Samia wakiongozwa na Geoffrey Okello na Cleophas Okisai ambao hulazimika kusafiri mwendo mrefu kutoka maeneo hayo hadi mjini Busia kuhudhuria vikao vya mahakama, huku mradi wa ujenzi wa mahakama ya Port Victoria, Funyula na Malaba ukikwama kwa zaidi ya miaka saba sasa.
“Wakazi wa Busia tumeteseka kwa miaka sasa tukitafuta huduma za mahakama. Hapo awali imetulazimu kusafiri kwa muda mrefu ili kutafuta haki,” alisema Geoffrey Okello mkaazi wa Budalangi.
Kwa mujibu wa wawili hao, wakazi wengi wamekuwa wakikosa kupata haki kutokana na umbali wa mahakama, hali hiyo pia ikipelekea kuongezeka kwa visa vya uhalifu na ufisadi.
Wakazi hao wanaomba idara ya mahakama kuharakisha ujenzi wa mahakama ndogo Funyula na Malaba ili kuwasaidia wakazi wote kupata haki zao kwa wakati unaofaa.
Na Absalom Namwalo