Sunday, December 22, 2024
Home > Counties > Bungoma > Superstars Yang’aa dhidi ya Transfoc Nyumbani

Superstars Yang’aa dhidi ya Transfoc Nyumbani

Kikosi cha soka cha Bungoma Superstars kilivuna ushindi mkubwa dhidi ya majirani zao Transfoc FC Jumapili hii na kupaa hadi nafasi ya kumi na tatu kwenye jedwali la ligi ya Super nchini.

Ushindi huo wa mabao mawili kwa moja katika uga wa uwanja ndege mjini Bungoma uliyafufua upya matumaini ya kikosi hicho kupambania nafasi kumi za kwanza kwenye mashindano hayo ya soka ya divisheni ya kwanza nchini kanda ya magharibi.

Kwa mujibu wa nahodha wa kikosi hicho Caleb Kiplagat aliyezungumza na KNA kwenye mahojiano ya moja kwa moja baada ya ushindi huo, kikosi hicho kiliweka masaibu yake kando na kuelekeza nguvu zake zote kwa mtanange huo.

Hata hivyo nahodha huyo pia akiwapongeza mashabiki waliojitokeza na kukishinikiza kikosi hicho kudhihirisha ubabe wake.

“Tumetoka mbali kwa sababu ukiangalia juma moja lililopita tulikuwa mkiani lakini nawashukuru wenzangu kwa kutia bidii na kujititimua misuli kuhakikisha kuwa kikosi chetu kinalitetea Jina Lake,” Kiplagat alikariri.

Kwa mujibu wa jedwali hilo mnamo Jumatatu ya tarehe nne mwezi huu, waburura mkia walikuwa Superstars kwa alama kumi na nne kabla ya kuandikisha sare dhidi ya G. D. C FC kule Nakuru Jumatano na kuwabamiza Transfoc hapo Jumapili matokeo yaliyowarudisha kwenye ramani ya ligi hio.

Kiplagat pia alieleza jinsi ushindi utawafaa wanangarambe hao katika mechi zao zijazo kwani wataingia ugani wakiwa morali pamoja na ubabe wa kipekee.

“Ama kweli Transfoc ni timu kubwa kwenye mashindano haya na ushindi wetu dhidi yao ni jambo la kutia moyo sana katika mechi zetu zijazo,” alisema Kiplagat.

Hata hivyo kikosi hicho bado kina kibarua kizito kwani kina miadi na Bondo United huko Siaya, Kamungei FC, Mayenje FC kabla ya kufunga udhia na mioto wa jiji la Kisumu Hotstars.

“Tutajitahidi kwa kadri ya uwezo wetu kuandikisha matokeo mazuri katika mechi zilizosalia,” Kiplagat asema.

Katika matokeo mengine ya kipute hicho ni kwamba vikosi vya Luanda Villa FC na Mayenje FC viliandikisha sare tasa nao G. D. C wakiwakalifisha na kuwabamiza Sunderland Keroche mabao matatu komboa ufe.

St. Joseph FC walipoteza nyumbani dhidi ya Kona Rangers mabao mawili kwa moja kabla ya Sindo FC kuirindima Kamungei bao moja mtungi.

Jumatatu tarehe kumi na moja ilikuwa zamu ya Nyota FC kuwavaa Green Commandos kwenye uga wa nyumbani.

Na Mwangi Oliver

 

Leave a Reply