Serikali ya Kenya na washirika wake wa kimaendeleo watatoa takriban shilingi bilioni 1.3 ili kuuendeleza mradi mkubwa wa unyunyizaji mashamba utakaotumia mvuto wa ardhi katika kaunti ya Tana River.
Serikali imetenga shilingi milioni 900 huku washirika wake wakitazamiwa kutuoa jumla ya shilingi milioni 369 katika mwaka huu wa kifedha ili kuiwezesha Bodi ya Kitaifa ya Unyunyizaji kuuendeleza mradi unaonuiwa kuukarabati mpango wa unyunyizaji wa Bura.
Bodi hiyo ya unyunyizaji maji imesema kuwa baadhi ya washirika wa kimaendeleo wanaotazamiwa kutowa fedha hizo ni Serikali ya Kuwait, Benki ya Uarabuni ya Maendeleo ya Kiuchumi Afrika (BADEA) na Hazina ya Maendeleo ya Kitaifa ya Nchi Zinazouza Mafuta Nje (OFID).
Tangazo hilo la Bodi ya Kitaifa ya Unyunyizaji linafuatia ziara ya Naibu wa Rais, William Ruto katika shamba la unyunyizaji la Bura katika kaunti ndogo ya Tana Kaskazini ambako Bw. Ruto alitangaza kuwa serikali itatoa shilingi milioni 900 kwa ajili ya kuuendeleza mradi huo.
“Serikali itatoa shilingi milioni 900 ili mradi huo ukamilike na kutuwezesha kutimiza agenda yetu ya usalama wa chakula nchini,” Naibu wa Rais alisema katika mji wa Bura.
Bw. Ruto alisema mradi huo, kati ya mingine, utaizidia serikali kutekeleza ajenda yake ya Mambo Manne Makuu, ambayo alisema ndiyo itakayoshughulikiwa sana na serikali katika miaka minne ijayo.
“Serikali itaongeza sana uwekezaji wake katika usalama wa chakula, makao rahisi, utengezaji wa bidhaa na afya kwa wote,” alikariri.
Utekelezaji wa mradi huo ambao ulianza miaka mitano na miezi tisa iliyopita bado uko kiwango cha asilimia 30 tangu kandarasi kati ya Bodi hiyo na kampuni ya IVRCL ya India ilipowekwa sahihi Februari 27, 2013.
Katika taarifa kupitia kwa barua pepe hivi punde, Bodi ya Unyunyizaji imethibitisha kuwa pamoja na shilingi milioni 900 zilizotangazwa na Naibu Rais, washirika wa kimaendeleo watatoa shilingi milioni 369 kuukwamua mradi huo ambao ungekamilika miezi 38 iliyopita.
Wawakilishi wa wakulima pamoja na maafisa wa NIB wamesema kukamilishwa kwa mradi huo kutapunguza kwa kiwango kukubwa gharama ya unyunyizaji na kuhakukisha mtiririko wa maji usiokoma katika mitaro ya unyunyizaji mashambani.
Ulipoanzishwa, mradi huo wa mabilioni ya shilingi ulisifiwa kama suluhisho la gharama kubwa ya unyunyizaji maji katika mpango wa unyunyizaji wa Bura, lakini utekelezwaji wa mradi huo umekua ukienda kwa mwendo wa konokono kwa takriban miaka sita.
NIB iliweka sahihi makubaliano na kampuni maarufu ya ujenzi ya India inayojenga miradi ya maji iitwayo IVRCL Infrastructure Limited tarehe 27 Februari, 2013. Mradi huo ulipaswa kukamilika katika muda wa miezi thelathini, na ungeanza kufanya kazi katika mwezi wa Septemba 2015.
Mhandisi Mkuu wa Unyunyizaji katika Bodi ya NIB, Alexander W. Kuria, katika ujumbe wa barua pepe, alithibitisha kuwa serikali ya kitaifa itatoa shilingi bilioni 900 mwaka huu, huku washirika wa kimaendeleo wa Kenya wakitoa shilingi milioni 369 mwaka huu wa kifedha.
Mhandisi Kuria anasema sababu kubwa iliyochangia kuchelewa kwa utekelezaji wa mradi huo ni pamoja na matakwa fidia kwa wenye ardhi ambayo hayakutarajiwa na ambayo yalichelewesha kuanzishwa kwa mradi kwa miezi 22. Wenyeji walidai kufidiwa kwa ardhi ambako mradi huo ulipaswa kupitia.
Pia anasema kampuni iliyopatiwa kandarasi hiyo ilichelewa kukusanya pamoja vifaa na mitambo iliyohitajika katika sehemu ya mradi, na kwamba serikali ya Kenya na washirika wake pia walichelewa kutoa malipo.
Kuria anasema kuwa NIB iko katika harakati za kumtafuta mwana kandarasi mwingine ili kuhakikisha ueleshwaji wa kasi wa mradi huo, kwani kandarasi ya awali ilisitishwa.
“Kandarasi kati ya NIB na IVRCL Limited ya India ilikatizwa baada ya kuanzishwa kwa kesi ya kufilisika kwa kampuni hiyo huko India, kulingana na makubaliano yetu,” anasema.
Bw. Kuria anasema mradi huo ni muhimu sana, kwani utapunguza vikubwa gharama ya uzalishaji kwa kukomesha matumizi ya mabomba kusambaza maji, ambayo huigharimu bodi hiyo kiasi cha shilingi milioni tano kila mwezi.
Anasema mradi wa kutumia mvuto wa ardhi ukikamilika utasaidia kupanua mashamba ya kunyunyiziwa maji kutoka ekari 12,000 hadi ekari 15,000 kwa kufungua ekari nyingine 3,000 huko Masabubu.
Anasema mradi huo pia utahakikisha kuweko kwa maji ya kunyunyizia kwa kutoa lita 1,100 kila sekunde moja mwaka kinyume na kiwango cha sasa cha lita 2,700 kwa sekunde kupitia mabomba.
Shamba la Bura lapatikana kandokando ya mto Tana, takriban kilomita 50 kaskazini mwa mji wa Hola, ambao ni mji mkuu wa Kaunti ya Tana River.
Kwa sasa shamba hilo hupata maji kupitia mabomba yanayoendeshwa na mafuta ya dizeli ambayo yana uwezo wa kusukuma lita 2,700 za maji kila sekunde.
Maji yanapoinuliwa kutoka mtoni huteremka kupitia mitaro inayopita kandokando mwa mashamba ambako wakulima hutumia mifereji midogo kuelekeza maji mashambani mwao.
Likianzishwa katika mwaka wa 1977, shamba la Bura likikuwa limelenga kuzipa makao familia 5,150 ambazo zingetumia hektari 6,700 za ardhi ya kunyunyizwa.
Hata hivyo miundo msingi iliyowekwa iliweza kuhudumia hektari 2,500 pekee kwa sababu ya vizuizi vya kifedha.
Hata hivyo, Bodi ya Unyunyizaji imesaidiwa na serikali ya Kenya kufungua ekari 12,000 katika mpango huo.
Mpango huo ulinuiwa kutumia mvuto wa ardhi kuelekeza maji mashambani lakini ukosefu wa fedha haukuliruhusu jambo hilo kufanyika wakati huo, ndipo ikaamuliwa itumiwe mabomba kama jambo la muda mfupi.
Hata hivyo, matumizi ya mabomba yanayotumia mafuta ya dizeli yamekuwa kikwazo kikubwa katika kuuendeleza mradi na kuupanua kwa sababu ya gharama kubwa ya kuidumisha mitambo hiyo na bei ya juu ya mafuta. Mitambo hiyo pia hufyonza mchanga na kuharibika.
Ili kusuluhisha tatizo hili, serikali ya Kenya iliweka sahihi katika mkataba wa mkopo na serikali ya Kuwait, BADEA na OFID mwaka wa 2008 kwa kuukarabati mradi huo ikiwa na lengo la kustawisha miundo msingi itakayowezesha maji kuteremka bila kutumia mitambo ya dizeli.
Mimea inayokuzwa katika shamba la Bura ni pamoja na mahindi, matikiti maji, vitunguu, nyanya na pamba kati ya mingine.
Mradi huu unajumuisha kujengwa kwa mahali pa kutolea maji katika nyanda za juu za mto Tana, kujenga mitaro mipya na kuikarabati ile iliyopo, kuzilinda kingo za mto, kati ya mambo mengine.
Na Emmanuel Masha