Thursday, November 14, 2024
Home > Counties > Bungoma > Mwanaume aliye na uvimbe aomba msaada

Mwanaume aliye na uvimbe aomba msaada

Mwanaume mmoja kutoka kijiji cha Mukhuyu, wadi ya Maraka eneo bunge la Webuye Mashariki kaunti ya Bungoma, anahitaji msaada wa shillingi takriban mia nne elfu (Sh400, 000) ili kufanyiwa upasuaji wa uvimbe kwenye kidevu chake.

Akizungumza na waandishi wa habari, Bwana Cyprian Otieno, mwenye umri wa makamo, alisema kuwa uvimbe huo ulitokana na kung’olewa jino.

Alisema kuwa mwaka wa 2019 baada ya kuhisi maumivu ya jino, alielekea katika hospitali ya wilaya ya Webuye ambapo alikutana na daktari wa meno na akamng’oa jino moja japo aling’oa jino ambalo halikuwa na shida.

Kutoka hapo baba huyu wa watoto wanne alianza kutumia dawa za kutuliza maumivu.

Mwaka wa 2020 mwezi wa nne, aligundua kuwa kuna uvimbe mdogo umejitokeza kwenye kidevu chake. Alitafuta dawa na kuanza kutumia ila uvimbe huo haukuisha.

Aidha alidokeza kuwa maumivu yalizidi na alilazimika kuacha kazi yake ya ufundi wa nyumba na kurejea nyumbani ambapo amekuwa akihangaika bila usaidizi wowote ikizingatiwa kuwa yeye ndiye alikuwa tegemeo la familia hiyo ya watu sita.

Akizungumza, bibiye Beatrice Nangila alikariri kuwa familia hiyo inapitia kwenye madhila baada ya mumewe kuugua.

Alisema mumewe alikuwa akigharamia karo ya watoto, kulipa kodi ya nyumba na mahitaji mengine ya ziada ila kwa sasa ufa unashuhudiwa katika familia hiyo.

Familia hiyo imetoa wito kwa wahisani mbali mbali akiwemo Gavana wa Jimbo la Bungoma Wycliffe Wangamati, mbunge wa eneo hilo Alfred Sambu na viongozi wengine kujitokeza na kuwapa mkono wa faraja ili Bwana Otieno ashughulikiwe kiafya.

Na Lydia Wafula

Leave a Reply