Monday, December 23, 2024
Home > Education > Mwanafunzi mmoja afariki huku wengine wakilazwa baada ya kuugua malaria

Mwanafunzi mmoja afariki huku wengine wakilazwa baada ya kuugua malaria

Mwanafunzi  mmoja wa kidato cha kwanza katika shule ya wasichana ya Sing’ore katikia kaunti ya Elgeyo Marakwet ameaga dunia baada ya kuugua ugonjwa wa malaria huku wenzake 5, wawili wao kutoka shule tofauti wakilazwa hospitalini.

Kulingana  waziri  wa afya katika kaunti hiyo, Kiprono Chepkok, yaonekana mwanafunzi huyo aliyejiunga na shule hiyo wiki jana, alikuwa tayari ameambukizwa ugonjwa huo kabla ya kuja shuleni.

Alisema wanafunzi wengine watatu kutoka shule hiyo pamoja na wengine wawili, mmoja kutoka St. Patricks na mwingine kutoka shule ya wasichana ya Mutei wanaendelea kupokea matibabu katika hospitali ya rufaa ya Iten.

Hata hivyo, Chepkok alisema serikali ya kaunti iko na dawa za kutosha kukabiliana na ugonjwa huo na kuwataka walimu kuwafikisha wanafunzi katika zahanati za afya pindi tu wanapoonyesha dalili za malaria ili washughulikiwe kwa haraka.

“Tunapata wanafunzi kutoka sehemu mbalimbali nchini wengine wakitoka maeneo ambayo hushuhudia visa vingi vya ugonjwa wa malaria na kwa hivyo ni muhimu walimu kuwa makini na kuhakikisha wanafunzi wanafikishwa hospitalini haraka iwezekanavyo,” alisema Chepkok.

Aliongeza kuwa maeneo ya bonde la Kerio yamekuwa yakiripoti visa vingi vya malaria na akawahakikishia wakazi kuwa zahanati zote za afya ziko katika hali ya tahadhari kukabiliana na ugonjwa huo.

Chepkok pia alisema wakazi katika maeneo ya nyanja za juu za kaunti hiyo hawafai kuwa na hofu ya kuambukizwa ugonjwa huo, huku akisema aina ya mbu anayesambaza ugonjwa wa malaria hawezi kuishi katika maeneo hayo.

Na  Alice  Wanjiru

Leave a Reply