Mwakilishi wadi katika bunge la Vihiga, Bi. Violet Bagada ameishukuru serikali ya gatuzi la Vihiga kwa uzindushi wa shughuli ya kuboresha miundo misingi katika chuo cha anuwai cha Keveya.
Bagada alitoa shukurani hiyo Jumamosi alipozuru chuo hicho kilicho katika gatuzi ndogo la Sabatia.
“Uboreshaji wa miundo misingi katika vyuo vya anuwai katika gatuzi letu kutachangia pakubwa sana katika kiwango cha masomo ya wanafunzi wetu,” alisema Bagada.
Mwakilishi wadi huyo aliorodhesha ukosefu wa madarasa ya kutosha, maktaba, mabweni na vyoo kuwa miongoni mwa changamoto ambazo vyuo vya ufundi vinakumbana nazo katika sehemu hiyo.
Hata hivyo, Bagada alimshukuru Gavana Willber Ottichilo kwa kile alichokitaja kama usimamizi bora wa fedha na rasilimali ya gatuzi laVihiga.
“Tangu Gavana Ottichilo achukue hatamu ya uongozi tumeshuhudia mabadiliko makubwa katika matumizi ya fedha za serikali ikilinganishwa na serikali ya hapo awali,” alikariri Bagada, huku akiwarai wenyeji kumpatia Ottichilo muda wa kutekeleza manifesto yake.
Mwana siasa huyo, alitumia fursa hiyo kuwahimiza wanafunzi katika chuo cha Keveye kusoma kwa bidii ili wahitimu na ujuzi utakaosaidia kuboresha hali ya kiuchumi na maendeleo katika gatuzi la Vihiga.
Siku ya alhamisi Gavana Ottichilo alikabidhi chuo hicho hundi ya shs.7, 800, 000 kwa wanafunzi 520 ambapo kila mwanafunzi alilipiwa karo ya sh.15, 000 na serikali ya gatuzi hilo.
Aidha gavana huyo alizindu rasmi shughuli ya ujenzi wa madarasa ya kisasa katika chuo hicho.
Na Wachira Josphat