Sunday, December 22, 2024
Home > Counties > Mtihani wa kidato cha nne  waingia siku ya pili bila pingamizi yoyote 

Mtihani wa kidato cha nne  waingia siku ya pili bila pingamizi yoyote 

Zaidi ya watahiniwa elfu tisa (9000) wa kidato cha nne (KCSE) katika kaunti ya Mombasa leo waliendelea na mtihani wao  bila usumbufu.

            Mitihani ya leo iliyoingia siku ya tatu inahusisha somo la hesabu na kemia. Zoezi la kuthibitisha mitihani hiyo lilifanyika katika jumba la Uhuru na Kazi mjini Mombasa mwendo wa saa kumi na mbili asubuhi.

            Mkurugenzi wa elimu katika kaunti ya Mombasa, Moses Bosire, alisema mitihani hiyo inaendelea vizuri bila matatizo.

            Bosire alisema kuna ulinzi wa kutosha na pia serikali inahakikisha kuwa maagizo yote ya kujikinga na maradhi ya corona yanafuatwa.

            Huku mtihani huo ukiendelea chini ya mikakati ya kuzuia ugonjwa wa Corona, waalimu wenye umri  zaidi ya miaka hamsini wameshauriwa kupokea chanjo ili kupunguza athari ya kuambukizwa virusi hivyo.

            Akizungumza wakati wa uzidunzi wa  mitihani hiyo nje ya makao makuu ya mkoa mjini Mombasa siku ya Ijumaa iliyopita, Mkurugenzi mkuu wa Tume ya kuajiri walimu (TSC) Dkt. Nancy Macharia aliwashauri waalimu wote wenye umri zaidi ya hamsini  kupata chanjo hiyo.

            Daktari Macharia alithibitisha kuwa waalimu 92,850 kutoka shule za umma na wenzao 16,500 kutoka shule za kibinafsi na kimataifa watapewa kipaumbele wakati wa shughuli hiyo ya kuchanjwa.

            Alisema kwamba tume ya waalimu imeteua wakufunzi 227,000 watakaoshughulika na michakato ya kusimamia mitihani hiyo.

            “Waalimu hao wamethibitishwa na baraza la mtihani kabla kuteuliwa kusimamia zoezi hilo,” alisema Daktari Macharia.

            Pia aliwapongeza waliohusika na mitihani ya KCPE kwa kuhakikisha kuwa mitihani hiyo ilifanyika kwa njia inayofaa lakini pia akatoa tahadhari kwa shule ishirini zinazoshukiwa kuwa na mipango ya ulaghai.

            Daktari Macharia aliwatakia watahiniwa wote kila la heri na kuwahimiza wanaosimamia mitihani kuwa waangalifu ili kuzuia juhudi zozote za udanganyifu.

            Pia, alihakikisha kwamba serikali imeweka mikakati ya kutosha, kuwalinda watahiniwa na wote wanaohusika na mitihani na maradhi ya corona kulingana na taratibu za Wizara ya Afya.

na Brian Kiprono/Mulu Elisha

Leave a Reply