Bi. Evarlyne Maiyo kutoka kijiji cha Kaplamai kaunti ndogo ya Keiyo Kaskazini aliwatayarishia wanawe chamchana, kisha baadaye mwendo wa saa kumi akaenda shambani kutafuta mboga za jioni kama ilivyo ada.
Haikuchukuwa muda mrefu aliposikia akina mama wakipiga mayowe, bi. Maiyo aliaacha shughuli yake ya kuchuna mboga mara moja na kukimbia mbio kuona yaliyokuwa yamejiri muda mchache tu baada yake kutoka.
“Nikiwa bado mbali niliwaona akina mama waliokuwa wakilia kwa sauti karibu na chimbo, niliona watoto niliowaacha wakicheza na mwanangu Samantha lakini sikumwona mtoto wangu, roho ilianza kunidunda,” alisimulia bi. Maiyo.
Alipofika, wale akina mama walimweleza kwamba mwanawe alitumbukia kwa chimbo walipokuwa wakicheza na wenzake. “Hapo hapo nilijua mwanangu ameshaaga dunia,” bi. Maiyo alisema kwa huzuni.
Majirani walifanya juu chini na kufaulu kuutoa mwili wa Samantha aliyekuwa na umri wa miaka miwili na nusu lakini licha ya juhudi zao, Samantha alikuwa amekata roho.
“Sikuamini, mtoto ambaye dakika chache nilikuwa naye, hata tukala na nikamwacha akicheza, sasa hayupo tena,” alisema kwa majonzi.
La kusikitisha ni kwamba chimbo lile lilichimbwa kwa shamba lao baada ya mumewe Alfayo Maiyo kulikodisha kwa wanakandarasi wanaojenga barabara mbali mbali katika kaunti ya Elgeyo Marakwet.
Hii ndio hali katika baadhi ya maeneo tofauti tofauti ya kaunti hii huku ujenzi wa barabara uliokuwa umengojewa kwa hamu ukiendelea. Kwa mujibu wa mpango-shirikishi wa maendeleo ya kaunti 2018-2022, (County Integrated Development Programme CIDP) kati ya kilomita 2,060.64 za barabara katika kaunti hiyo ni asilimia kumi tu ambazo zimewekwa lami.
Kutokana na haya, serikali kuu na ile ka kaunti zimejizatiti kuona kwamba hali hii imebadilika kwa kuwekeza mabilioni ya pesa kuimarisha barabara ikizingatiwa kwamba uimarishaji wa barabara ni kichocheo cha ukuaji wa uchumi na maendeleo.
Licha ya manufaa yanayopatikana kutokana na kuimarishwa kwa miundo msingi, hili pia limegeuka na kuwa kero kuu kwa wakazi. Hii ni kwa sababu wanakandarasi wanaojenga barabara hutia sahihi mikataba ya kuchukua mchanga kutoka kwa mashamba ya watu binafsi bila kuhusisha maafisa wa serikali.
Haya ndio yaliyompata Maiyo ambaye kwa sasa amebaki akilia baada ya kumpoteza mwanawe huku shamba alilokuwa akitegemea kuchuma riziki likibaki shimo ambalo hawezi kuziba.
Maiyo alisema mwanawe hakuwa wa kwanza kufa katika machimbo akisema wengi wamepoteza maisha yao katika machimbo mbali mbali katika eneo hilo.
Maiyo alisema alimshauri mwanakandarasi aliyekodisha shamba lake dhidi ya kuchimba kina kirefu lakini ushauri wake uliambulia patupu.
“Tunaomba serikali hasa ya kaunti kuingilia kati na kutusaidia kuziba machimbo hayo kwa sababu yataendelea kuhatarisha maisha si tu ya binadamu bali pia wanyama.
Hata hivyo kulingana na afisa wa shirika linalosimamia mazingira nchini (NEMA) Patrick Osale, wengi wa wakazi hawahusishi shirika lake wanapotia sahihi mkataba wa kukodisha mashamba yao na badala yake huja kulalamika baadaye.
“Wengi hutia sahihi bila kuelewa yaliyomo na huja kulalamika baada ya mwanakandarasi kwenda zake na kuwaachia machimbo ambayo hawajui wafanyie nini kwani hawawezi kumudu gharama ya kuyafunika,” alisema Osale.
Afisa huyo alisema wengi hulipwa kati ya sh.30,000-50,000 kwa ekari ilhali huenda ikawagharimu mamilioni kulijaza chimbo lile kwani mwenye shamba atahitaji vifaa ambavyo hana, kama vile malori ya kusafirisha mchanga.
Kulingana na sheria, afisa huyo alisema ni jukumu la mwanakandarasi kuhakikisha kwamba machimbo yote aliyochimba yamefunikwa akisema hili linaweza kufanyika kwa kuchukua udongo anaochimba barabarani na ambao hauhitaji na kumwaga kwa chimbo analotoa mchanga wa ujenzi.
Aliendelea kusema kwamba kabla ya kuanza uchimbaji, ni lazima eneo hilo lifanyiwe ukaguzi na kutoa ripoti ya athari kwa mazingira (Environmental Impact Assessment Report) akisema wengi wa wanakandarasi wanakwepa hili kwani hawataki kugharamia.
Hivyo basi anawashauri wakazi kuhakikisha wameihusisha afisi hiyo kabla ya kutia sahihi mkataba wowote na wanakandarasi akisema hili litawapa maafisa mamlaka ya kukagua yanayoendelea ili kuepuka janga. Alisema machimbo haya ni hatari hasa wakati huu wa mvua kubwa kwani yanajaa maji na pia hayajazingirwi na ua lolote.
Alisema tatizo hili halipo tu katika kaunti ya Elgeyo Marakwet bali ni la kitaifa akisema ni vizuri kuwa na sera kwamba mamlaka ya ujenzi wa barabara kuu (KENHA) iwe ikibaki na fedha za kukarabati machimbo yanayowachwa wazi kwani yana athari kubwa kwa mazingira bali na kuhatarisha maisha ya watu na wanyama.
Aliendelea kusema hili pia linazidisha hatari ya maambukizi ya ugonjwa wa malaria kwani yanatoa mazingara ya kuzaana kwa mbu na pia magonjwa mengine yanayotokana na maji chafu.
Na Alice Wanjiru