Chama Cha Kiswahili Afrika Mashariki (CHAKAMA) kinanuia kubuni baraza za Kiswahili hapa Afrika Mashariki ili kueneza ushirikiano na kukuza lugha.
Akizungumza katika chuo kikuu cha Maasai Mara mjini Narok katika kongamano la wataalamu wa Kiswahili kutoka Afrika Mashariki mnamo Ijumaa, mwenyekiti wa CHAKAMA Dkt. James Ontieri alisema kuwa baraza za Kiswahili zitapanua mipaka ya Kiswahili katika bara la afrika ili kuiendeleza lugha hii and kupanua mawasiliano.
“Nafasi ya Kiswahili inafaa kutetewa vikali ili kufanikisha ustawi wa lugha katika vizazi vya sasa na vijavyo,” Ontieri ambaye ni mhadhiri wa Chuo Kikuu Cha Maasai Mara alisema.
Vile vile, aliongeza kusema kwamba lugha ya sheng ambayo ni msimbo inayotumika hasa na vijana wa mitaa duni inatarajiwa kutafutiwa sheria na wasomi wa Kiswahili kwa kuzamia katika suala hilo na kutafuta namna msimbo huo wa sheng utatumika bila kuadhiri mazunguumzo ya lugha ya Kiswahili.
Mwandishi maaruufu Wallah Bin Wallah ambaye amebobea katika uandishi wa nakala za Kiswahili na viatabu vingi ambavyo vimetumiwa katika shule zetu aliwarai wanafunzi kujifunza lugha ya Kiswahili huku wakiwa wachanga ili watakapokuwa wakubwa watakuwa weledi na magwiji katika fasaha ya Kiswahili.
Akizumgumza kuhusu mtaala mpya, Wallah alisifu mfumo huo huku akisema kuwa mtaaala huo utamwezesha mwanafunzi kutumia mbinu zozote kwa kutegemea maarifa yake binafsi tofauti na na hapo awali ambapo walimu walikuwa wanafunza bila kutaka kufahamu uwezo wa kila mwanafunzi.
“Mfumo mpya huu wa elimu utafaulu na kunawiri endapo tu, watekelezaji watautekeleza jinsi mpango na taratibu unavyotakikana,” wallah aliongezea.
Kongamano hili la siku mbilii lilihudhuriwa na wataalamu waliobobea katika lugha ya Kiswahili kutoka mataifa manne ya afrika mashariki ambayo ni Kenya,Uganda,Tanzania na Rwanda huku wakitarajiwa kuchagua viongozi wapya wa CHAKAMA hapo kesho .
na Mabel Keya