Kufuatia kuongezeka kwa gharama ya maisha nchini, wanachama wa kundi la Bidii na Kazi kutoka kijiji cha Mida katika kaunti ya Kilifi, wamehimiza kina mama wote kukumbatia kilimo hai ili kukidhi mahitaji ya mboga katika familia zao na kupunguza uhitaji wa pesa katika matumizi ya nyumbani.
Wanachama wa kundi hilo wakiongozwa na Gladys Kenga wanasema kina mama wanaweza kutumia mbinu za kilimo hai kupanda mboga kama vile sukuma, mchicha, nyanya na vitunguu kwa urahisi mahali popote ili kupunguza gharama, hasa wakati huu ambaop familia nyingi zinahangaika.
Katika mahojiano na wanabari katika kijiji hicho, Bi Kenga ambaye ni mwanachama anayenufaika pakubwa na maarifa hayo, alisema kwa miezi kadhaa sasa hajakuwa na haja ya kuenda sokoni kwa sababu anavuna mboga za kutosha kwenye kiwanja chake.
“Mchicha, sukuma, tomato niko nazo, kwa hivyo siendi sokoni kununua mboga, nachukua pale nyumbani natumia.
Kwa hivyo nimeona manufaa kutokana na mradi huu. Hata natamani elimu hii ningekua nayo kitambo, singetumia pesa,” alisema.
“Ningetaka kusema wamama wenzangu sisi tumetegemewa sana nyumbani. Ukiwa na elimu hii ya kupanda kwako nyumbani, ile pesa ambayo ungetumia kununua mboga, inakusaidia kwa mambo mengine,” Kenga aliongeza.
Aidha alisema mbinu za kisasa za kuzalisha mboga nyumbani hazina gharama nyingi kwani hutumia maji kidogo ya jikoni.
Kenga alidokeza kwamba kina mama wengi katika kijiji cha Mida sasa wamegeukia kilimo hicho cha kisasa na wamesaidika katika kuzikimu familia zao.
“Hapa kijijini kwetu ukiingia katika kila boma utakuta kila mmoja yuko na gunia lake pale kando ya mlango wa jiko anaweka mboga zake kwa sababu watu wengi wamekuja kuchukua hii elimu hapa kwetu chamani,” alisema.
Vilevile, alisisitiza kuwa kina mama wanaoishi mijini pia wanaweza kufaidika na mradi huu kwani hauhitaji nafasi kubwa na unaweza panda mboga hata nje ya mlango.
Mbali na matumizi ya nyumbani, Salma Abdalla, ambaye pia ni mwanachama wa kundi la Bidii na kazi alisema kilimo hai kimewasaidia kupata mapato madogomadogo kwani watu kutoka vijiji jirani hufika kwao kununua mboga.
“Imetusaidia sana kwa sababu haiko na gharama nyingi. Gunia moja la mchanga unaweza panda mchicha ukatoa kama mia nne na gunia umenunua shilingi hamsini. Tukiwa na mteja anataka mboga mbali na hotelini tunaweza kumuuzia,” alisema.
Hata hivyo, wanachama hao walieleza kuwa changamoto kubwa wanayopitia ni mifugo wa nyumbani ambao mara nyingi huvamia na kuharibu mboga zao hivyo wanaomba msaada wa nyaya za stima ili kuzuia wanyama.
Na Jackson Msanzu