Sunday, December 22, 2024
Home > Editor Picks > Kaunti ya Mombasa kuzindua mikakati ya Kuboresha usalama barabarani

Kaunti ya Mombasa kuzindua mikakati ya Kuboresha usalama barabarani

Kaunti ya Mombasa imetangaza mpango wa kuondoa mabasi yote ya abiria yanayohudumu kutoka katikati mwa jiji kusafirisha watu hadi kaunti jirani ili kupunguza msongamano wa magari unaoshuhudiwa maeneo hayo.

Kulingana na Afisa Mkuu wa Usafiri kaunti hiyo, Ali Sharif, kituo kikubwa cha mabasi kitajengwa katika eneo la Kibarani ambapo abiria watalazimika kuchukua teksi au matatu ili kuingia jijini.

Isitoshe, serikali hiyo kupitia ufadhili wa Serikali ya Taifa ya Japan, inalenga kuanzisha mfumo wa usafiri wa kutumia teknolojia ya kisasa kwa kuweka maboya ya trafiki 22 ndani ya jiji la Mombasa na kituo cha udhibiti wa trafiki.

Sharif anasema kwamba mradi huo unatarajiwa kuanza mapema mwakani punde tu fedha za ufadhili zitakapoidhinishwa na shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Japan.

“Kati ya miradi tunayotaka kufanya ni miongoni mwa mifumo bora ya usafiri na kujenga na kufunga ishara za trafiki 22 katika mji wa Mombasa, hasa katika kitengo kikuu cha biashara,” alisema Sharif.

Aliongeza kwamba ishara hizo zitakua na chapisho la ishara tatu za ujumbe tofauti ambazo zitatumika kupitisha ujumbe kwa abiria na wendeshaji magari na bodaboda.

Vile vile kaunti ya Mombasa inalenga kuunda kituo cha udhibiti wa trafiki cha hali ya juu.

Sharif ameongeza kwamba serikali ya kaunti inafanya kazi pamoja na NTSA kuanzia mwaka 2022 kuhakikisha barabara ziko salama.

“Ufadhili huu utatusaidia sisi katika kushugulika kuweka vivukio vya watu, matuta ya kasi ili wananchi waweze kutumia barabara kwa usalama.

Wendeshaji magari wameombwa kupunguza kutumia barabara kwa kasi hasa msimu huu wa sherehe za krismasi unapowadia.

Aidha mkuu huyo wa usafiri alisema wataongeza idadi ya taa za mitaani haswa msimu huu wa Disemba ambapo shamra shamra za sikukuu ya krismasi zikiwadia.

Afisa huyo amesema serikali ina nia na madhumuni ya kupunguza msongo wa magari ndani ya mji wa Mombasa.

Haya yanajiri huku waandishi habari, umma na madereva wakiendelea kuhamasishwa kuhusu udumishaji wa usalama barabarani na serikali ya kaunti ya Mombasa kupitia shirika la Bloomberg Philanthropists.

Kevin Ismael, Mratibu wa Mawasiliano katika shirika hilo amesema kwamba wamekuwa wakifanya kazi na kitengo cha polisi cha nchi ili kujenga uwezo na kuendesha mazungumzo yenye yataweza kuwawezesha, kuwajibika na kufanya kazi yao vile inavyofaa.

Ismael amesema kwamba wana mpango wa kuzindua kampeni kwenye vyombo vya Habari ambayo italenga waendeshaji tuktuk na matatu ambao maswala ya kupeleka gari kwa kasi yanawalenga.

Vile vile, afisa huyo amehimiza umuhimu kwa waandishi wa Habari kutumia mfumo wa uhandishi wa kutoa suluhisho katika kuripoti habari.

“Ni muhimu zaidi kuweza kuzingatia na kubadilisha namna ya vile tunaripoti maswala ya usalama barabarani. Sisi kama shirika lengo letu kubwa ni kupeana msaada wa kiufundi kwa serikali ya kaunti, NTSA na wale wote wanaohusika na maswala ya usalama barabarani,” alisema Ismael.

Aliongeza ya kwamba shirika hilo limekuwa likifanya mazungumzo ya jinsi wanaweza kuwawezesha kimaisha waendeshaji wa tuktuk ambao ni wengi katika mji wa Mombasa.

Kwa upande wake, msimamizi wa NTSA nchini Bw Samuel Musumba amesema kwamba lengo lao ni kuongoza wanaotumia barabara kufika mwisho wa safari yao salama na kwa kasi inayofaa na wala sio kuwakamata.

Vile vile amesema msimu huu wa sherehe kutaongezeka kuwepo kwa ukaguzi wa magari kutathmini kama yako na stakabadhi husika hasa magari yanayobeba abiria.

“Kama nchi, tungependa tupunguze visa vya ajali barabarani kwa njia zozote zile. Tunaomba wananchi kuripoti visa vya madereva kukiuka sheria barabarani kwa nambari zetu ambazo ziko wazi, wanaweza tupigia simu ama kuwasilisha ujumbe mfupi tuchukulie madereva hawa hatua,” aliongeza.

Amewaonya abiria kutopanda gari iliyojaa na kuwakumbusha kwamba hakuna anaeshurutishwa kupanda gari lililojaa hivyo kuwaonya abiria watakaoshikwa kwamba sheria itafuata mkondo wake.

Na Chari Suche

Leave a Reply