Sunday, December 22, 2024
Home > Education > Kasisi awashauri wazazi

Kasisi awashauri wazazi

Wazazi wameshauriwa kuwa na uhusiano wa karibu na watoto wao, ili kuwasaidia kukabiliana na athari chungu nzima za mitandao ya kisasa ambazo zinaweza kuwakumba na kuhatarisha maisha ya usoni.

Kasisi Peter Kariuki, kutoka kanisa ya Newlife katika kata ndogo ya Kikuyu, alisema kuwa ni sharti kuwe na uhusiano mzuri nyumbani ili kuwezesha kizazi kipya kuwa na mwelekeo katika maisha yao.

Kariuki alitoa mawaidha haya mnano Jumapili baada ibaada ya ibada ya vijana iliyoandaliwa na kanisa lake ili kuwapa vijana wosia mwema hasa wakati huu wa likizo.

Alisisitiza kuwa mifumo mipya ya kiteknolojia haina ubaya bali inafaa kutumiwa kwa njia inayofaa.Alitoa mfano wa hivi maajuzi ambapo baadhi ya vijana potovu walitumia mitandao ya kijamii kutuma picha chafu jambo lililozua hofu miongoni mwa wazazi.

Katika mahojiano ya kipekee na KNA, kasisi huyu ambaye pia ni mshauri wa vijana alisema wazazi wamelegeza kamba kwa kuruhusu watoto kutumia mitandao ya kijamii wakati wo wote na kuwazoesha maisha ya starehe ambazo zimepita mipaka ya maadili mema.

Kariuki alilalamikia tabia ya vijana wa siku hizi kukimbilia kuiga wazungu na desturi zao ambazo ni tofauti kabisa na mila za kiafrika.

Isitoshe, wazazi hawaonekani kushughulikia mabadiliko ya kitabia miongoni mwa watoto wao jambo ambalo mwishowe husababisha madhara makubwa katika jamii.

Kutokana na ulegevu miongoni mwa wazazi, watoto siku hizi wanaishia kutafuta ushauri kutoka kwa wanarika wenzao ambao wanawapotosha hata zaidi.

“Kwa kiwango kikubwa wazazi wamewaachia walimu wajibu wao wa malezi bora wautekeleze pamoja na ule kutoa mafunzo,” Kasisi huyu alizidi kueleza.

Kulingana na Kariuki, hapo zamani mambo yalikuwa tofauti kwani kila mtoto alichukuliwa kama mali ya jamii na kila mtu mzima angemwadhibu mtoto wa mwenzake mradi kulikuwa na makosa.

Hata hivyo, kwa sasa ni kila mtu na mtoto wake na ile nidhamu ya kijamii imetoweka.

Kasisi huyu alimalizia kwa kuwashauri wazazi kuwaelekeza watoto wao ili taifa liwe na viongozi wa kutegemewa siku za usoni.

Na  Winnie  Kimani

Leave a Reply