Monday, December 23, 2024
Home > Counties > Kadhi mkuu ashauri waislamu kufuata msharti ya serikali kujikinga na virusi vya korona

Kadhi mkuu ashauri waislamu kufuata msharti ya serikali kujikinga na virusi vya korona

Kadhi Mkuu nchini Kenya Sheikh Ahmed Muhdhar ametoa mwito kwa waumini wa Kiislamu kufuata masharti ya serikali ya kujikinga na virusi vya korona wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhan.

Sheikh Muhdhar alisema lazima waislamu waelewe kuwa ni jukumu la kila mtu kusaidia katika juhudi za kuzuia kuenea kwa virusi hivyo ambavyo vimesababisha maafa na taharuki duniani kote.

Mwezi mtukufu wa Ramadhan ambao ni nguzo ya nne katika nguzo tano za dini ya Kiislamu unatarajiwa kuanza mwishoni mwa wiki ijayo.

Katika mwezi huo waislamu kote ulimwenguni hujizuia kula na kunywa, kuzidisha ibada na pia kuwasidia wale wasiojiweza katika jamii.

“Ijapokuwa mwezi mtukufu wa Ramadhan ni ibada muhimu itatulizimu kubadili tabia zetu na kufuata masharti yaliyotolewa na wizara ya afya ili kijikinga na janga la corona,” alisema Shiekh Muhdhar wakati wa mahojiano na KNA mnamo Jumamosi huko Mombasa.
Alisema masharti yaliowekwa na serikali ya kudumisha usafi na kuepuka kutangamana ni kwa faida ya wakenya wote.

Kadhi Mkuu alisema, “itabidi waislamu wafanye ibada zao majumbani kwao ili kuepuka mikusanyiko ya watu ambayo inaweza kusababisha kuenea kwa virusi vya korona.

Sheikh Muhdhar alisema haitawezekana kwa serikali kuondoa au kulegeza masharti yaliyoko kama vile kufunga nyumba za ibada na amri ya kutotoka nje ili kupunguza kasi ya kuenea kwa virusi hivyo.

Siku ya Jumatano, viongozi kadha wa kiislamu wakiwemo maimamu na wabunge waliomba serikali kuongeze muda wa kutotoka nje kuanzia saa nne usiku hadi saa kumi na moja alfajiri na pia kufunguliwa kwa misikiti wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhan.

Wakiongozwa na baraza la maimamu nchini (CIPK), viongozi hao walisema watahakikisha masharti yote yaliowekwa na wizara ya afya yanatekelezwa kikamilifu ili kuhakikisha waumini wanajilinda na virusi ya korona.

Hata hivyo, Sheikh Muhdhar alisema haitawezakana kwa masharti hayo kuondolewa kwa sasa kwa sababu ya hatari ya kuenea kwa virusi hivyo.

Alisema hali hii ni ya muda tu na kuwataka waislamu kuunga mkono juhudi za serikali za kuzuia kuenea kwa virusi vya korona.

Hadi sasa wakenya 246 wamethibitishwa kuwa na virusi vya korona, huku wengine 11 wakiaga dunia kutokana na maradhi hayo.

Na Mohamed Hassan

Leave a Reply