Wednesday, December 25, 2024
Home > Counties > Kiambu > Jaji mwanzilishi wa mahakama atetea washtakiwa

Jaji mwanzilishi wa mahakama atetea washtakiwa

Kiambu, Ijumaa Aprili 20, 2018 KNA na Lydia Shiroya

Jaji Mkuu wa mahakama ya Kiambu anayeondoka Joel Ngugi ameomba mahakama za humu nchini kusikiliza kesi kwa ukamilifu ili ziweze kutoa uamuzi wa busara unaokubalika na pande zote mbili.

Kiambu
Jaji wa Kiambu Joel Ngugi (katikati) ambaye amepata uhamisho hadi mahakama kuu ya Nakuru.
Kulia ni Stella Atambo ambaye ni hakimu mwandamizi na George Njoroge, karani mkuu wa mahakama ya Kiambu.

Ngugi alisema haya Alhamisi alipokuwa akifunganya virago kutoka ofisini mwake katika harakati za kuhamia katika Mahakama Kuu ya Nakuru alikohamishiwa mwezi uliopita.

“Washtakiwa ni binadamu wenzetu, wako na hisia na haki zao zinapaswa kuheshimiwa,” Ngugi alisisitiza.

Jaji huyu daima huwa mcheshi katika kazi yake na kabla ya kuanza kusikiza kesi yo yote, anajulikana kumtuliza mshtakiwa kwa kumsalimu kwa jina lake, kisha anamkaribisha na kumuuliza ikiwa angependa kuketi au kusimama wakati wa kusikiza mashtaka.
Isitoshe, Ngugi pia huwauliza washtakiwa ikiwa wangependa kupewa maji ya kunywa au chai ndiposa waendelee na kikao katika makahama kuu ya Kiambu.

Aidha washtakiwa wanaohitaji huduma za wakalimani huwa wanapewa nafasi ya kushirikisha watu wanaoielewa lugha ya Kiswahili, lugha ya mama au nyingine yo yote kulingana na matakwa yao.

Akizungumza na shirika la habari la KNA baadaye, Ngugi aliwasihi wafanyi kazi wa serikali kuwa watiifu kwa muajiri wao.

“Mimi nimefanya kazi Kiambu tangu 2016 na sasa naelekea Nakuru na Jaji Mkuu akisema niende Pwani au Magharibi, nitakubali bila kuuliza maswali kwa vile ni mimi niliomba kazi na niko tayari kuwatumikia Wakenya wote”, alisema huku akiangua kicheko.

Ngugi ambaye ni mwanzilishi wa mahakama kuu ya Kiambu iliyofunguliwa Juni moshi, 2016 aliwashauri waajiriwa hao kuwa tayari kufanya kazi katika sehemu zote nchini kwa sababu waliapa walipoingia kazini kuwa wangehudumu mahali po pote nchini.

Akirejelea utenda kazi katika mahakama ya Kiambu, Ngugi alisema kuwa alipenda kazi yake na pia alikuwa ameweka msingi thabiti ambao uliwawezesha wakaaji wengi kuwa na imani na mahakama hiyo.

“Nitaishi kukumbuka Kiambu na namtakia atakayechukuwa wadhifa wangu kila la heri katika kazi yake,” alinena.
Wakati wa sherehe hizo, Bi.Stella Atambo ambaye alimwakilisha hakimu mkuu wa mahakama ya Kiambu Bi.Patricia Gichohi alimmiminia sifa Jaji anayeondoka huku akisema alikuwa na uhusiano mzuri na kila mmoja; mkubwa kwa mdogo.

Jaji Christine Meoli anatarajiwa kuchukuwa nafasi ya Ngugi ifikiapo Mei 7, baada ya kupata uhamisho kutoka mahakama ya Milimani katika Kaunti ya Nairobi.

Miongono mwa kesi nzito ambazo Ngugi amewahi kusikiza ni ile ya kijana ambaye alituhumiwa kumuua dadake aliyekuwa mwanafunzi katika chuo kikuu cha JKUAT mwaka wa 2016 na ile ya mwalimu mkuu wa shule ya wasichana wa Ichachiri anayetuhumiwa kwa kumuua mume wake mnamo Disemba 2016.

Katika kesi ya kwanza, Ngugi alimfunga kijana mhusika miaka mitatu alipotoa uamuzi wake huku akisema kuwa mshtakiwa alikuwa amejutia kitendo hicho.

Kesi ya mwalimu Jane Muthoni Mucheru haijaamuliwa, na mshtakiwa amewahi kumwambia Jaji Ngugi ajiondoe kutoka kwa kesi hiyo kwa vile alimfunga mshtakiwa mwenza miaka saba alipotoboa walivyokodiwa na kulipwa na mshtakiwa ili kutekeleza unyama huo.

Leave a Reply