Maafisa wa IPOA waendelea kuzuru vituo mbalimbali vya kupiga kura Kaunti ya Laikipia kuhakikisha kuwa maafisa wa usalama wanatekeleza majukumu yao ipasavyo.
Kulingana na naibu mwenyekiti wa shirika la IPOA Daktari Jonathan Lodompui, alisema kuwa wamezuru vituo mbalibali vya uchaguzi ili kutathmini utendekazi wa maafisa wa usalama kwa lengo la kuhakikishia wananchi kuwa wamo salama.
“Hakuna ripoti yoyote tumeandikisha kuhusiana na swala la ukosefu wa usalama,” asema Dkt. Lodompui.
Mgombea wa kiti cha Useneta Kaunti ya Laikipia Thuita Mwangi, amewapongeza washikadau kama maafisa wa IEBC, walinda usalama ambao wamejitolea mwanga ili kufanikisha shughuli nzima ya uchaguzi. Aidha amewashukuru wananchi kwa kukubali wito kujitokeza kupiga kura.
“Nawapongeza maafisa wa IEBC kwa kuwasaidia wakongwe, waliona mahitaji maalum na wajawazito katika kuingia kwenye vituo kwa njia ya utaratibu,”asema Bw. Mwangi.
Afisa msimamizi wa IEBC Cecilia Muthoni alizungumzia baadhi ya changamoto ambazo wamekabiliana nazo katika mchakato wa uchaguzi zikiwemo alama za vidole kutodhihirika kwenye mashine.
“Tumepata changamoto ya alama za vidole kutodhihirika katika machine hasa kwa wakongwe na wanaofanya kazi ngumu za mikono ila tumeweza kutumia kitambulisho pamoja na picha ya mhusika ili kuhakikisha kuwa hakuna anayeachwa inje katika shughuli hii muhimu,” asema Bi. Muthoni.
Aidha, wananchi wamepongeza maafisa wa usalama na IEBC kwa kuwaelekeza ipasavyo bila dhuluma yoyote.
Na Naomi Mokeira, Martha Wanjiru na Mauline Gesare