Kamishna msaidizi wa eneo la Elburgon katika gatuzi dogo la Molo katika kaunti ya Nakuru Mary Mwikabwe amewaonya vikali wakazi wa sehemu hiyo dhidi ya kuchezea kwenye reli iliyosalia ikining`inia baada ya daraja kuharibiwa na mvua kubwa iliyonyesha katika eneo hilo.
Bi Mwikabwe alisema kuwa anasikitishwa kuona watu wazima pamoja na watoto wakichezea hapo jambo ambalo linahatarisha maisha yao.
Kamishna huyo msadizi aliendelea kusema kuwa licha ya kujaribu kuwafukuzwa na kuonywa na viongozi wengineo, wanaendelea kupuuza na kuendelea kuingia kwenye reli hiyo.
Mkazi mmoja wa kujitolea wa kuelimisha jamii kuhusiana na maswala ya afya, James Kiiru anadai kuwa kuwafukuza hapo kumegeuka kuwa mchezo wa paka na panya kwani pindi tu maafisa wa polisi wanapotoka huko, wao hurundikana tena huku wengine wakionekana kuivuka reli hiyo inayoning’inia.
Bwana Kiiru aliwashauri wakazi wa eneo hilo kutii agizo la viongozi wa kijiji pamoja na maafisa wa usalama na kukoma kuchezea hapo kabla ya maafa kutokea.
Kutokana na mvua kubwa inayoendelea kunyesha, daraja hilo lilizidiwa na nguvu za maji na hivyo basi kuanguka na kuiacha reli pekee ikining’inia.
Na Emily Kadzo