Familia moja kutoka eneo la Nyakinyua, Kuresoi Kaskazini, kaunti ya Nakuru iliyokuwa imekabiliwa na hali ngumu ya njaa kiasi cha watoto kupika kinyonga sasa wana furaha riboribo baada ya serikali ya kaunti kuwanusuru na kuwapa tabasamu tena.
Kupitia taarifa yake iliyosomwa na msimamizi wa wadi hii, Nicholas Kiplagat, Gavana Susan Kihika alisema kuwa mama yao atapata kazi katika Idara ya Mazingara ya kaunti na vile vile watajengewa nyumba na kupata msaada wa chakula na mavazi hadi pale atakapoanza kupokea mshahara.
Isitoshe, watoto wake watahitajika kwenda shule ya kushughulikiwa mahitaji mengine.
Jane Chepng’etich ambaye ni mama wa watoto tisa, hakuficha furaha yake na kuishukuru serikali ya kaunti kupitia gavana kwa utu waliowafanyia akiongezea kuwa atajitahidi kazini ili kuwalea wanawe inavyopaswa.
Hapo jana jioni walipokea chakula, vitanda, magodoro na vifaa vinginevyo.
Watoto hawa wawili wa umri wa miaka 4 na 2 pia waliruhusiwa kwenda nyumbani kutoka hospitali ya gatuzi ndogo la Molo walimokuwa wamelazwa na serikali ya kaunti iliaahidi kufuatiliwa hali yao ya afya katika hospitali moja mjini Nakuru ili kuhakikisha kuwa wako salama salmin kiafya.
Ndugu yao wa umri wa miaka saba aliwatayarishia mlo wa kinyonga na kuchanganya na viazi ili angalau wapate lishe baada ya kushinda siku mbili bila kula chochote.
Wakati wa tukio hilo, Chepng’etich alikuwa ameenda kutafuta kibarua lakini aliporudi nyumbani, aliwapata watoto hao wachanga wakisokotwa na tumbo, kuendesha na kutapika.
Bila ya kupoteza muda walipelekwa katika kituo cha afya kilichokuwa karibu lakini wakaelezewa kuwa itakuwa bora iwapo watawafikisha katika hospitali ya gatuzi ndogo la Molo kwa matibabu zaidi ambapo walishughulikiwa kikamilifu.
Na Emily Kadzo