Familia moja kutoka eneo la Matumaini, gatuzi dogo la Molo sasa wanaomba msaada baada ya kujaliwa mabinti watatu kwa mara moja.
Kwa mujibu wa mama ya watoto hawa aliyejifungua jana katika hospitali ya gatuzi dogo la Molo, Sharon Alivinza wa miaka 27 alikiri kuwa familia yake imejawa na furaha kwa baraka hii kutoka kwa Mola lakini wasiwasi wao ni hali ngumu ya maisha itakayowawezesha kuwalea watoto wale bila shida yoyote.
Alivinza alisema kuwa katika kipindi cha mchipuko wa ugonjwa wa Korona, yeye pamoja na mumewe walipoteza kazi na wamekuwa wakifanya kazi za hapa na pale ili kuweza kuwalea wanawao watatu ambao ni wavulana wawili na msichana mmoja.
Kwa sasa, tegemeo lao ni mumewe anayefanya kibarua na hivyo basi itakuwa vigumu kwao kuwalea wanawao sita wanaohitaji mavazi, matibabu, chakula pamoja na mahitaji mengineo.
Kulingana na muuguzi Patricia Bett, Alivinza alijifungua salama watoto watatu lakini atasalia hospitali baada ya watoto wawili kuwa chini ya uzani unaostahili.
Bett alisema kuwa walikuwa wa kilo mbili, 1.7 na 1.3 hivyo basi kulazimika kuwaweka wawili wa mwisho walio na uzani wa chini ya kilo mbili katika kiangulio.
Hata hivyo, alihakikisha kuwa malaika hawa wako salama kiafya na wataendelea kuwa katika uangalizi wa madaktari hospitalini hadi pale watakaporuhusiwa kwenda nyumbani.
Aidha, aliwaomba wahisani kuwasaidia wanapoweza ili kuwawezesha watoto hawa kupata maziwa maalum na usaidizi wowote wanaoweza kujitolea.
Mkewe mbunge wa Molo aliyemtembelea Alivinza hospitalini, Winnie Kimani alimpa msaada wa maziwa ya watoto pamoja na vitu vingine vitakavyo iwezesha familia kuwalea watoto.
Na Emily Kadzo / Derrick Obiero