Mkuu wa kaunti ya Elgeyo Marakwet, Dkt. Ahmed Omar amewahakikishia wakazi wa Pokot Magharibi kwamba ng’ombe wote walioibwa juzi na vijana kutoka kaunti ya Elgeyo Marakwet watarudishwa.
Mkuu huyo alisema serikali itafanya kila juhudi kuona kwamba amani ambayo imekuwa ikishuhudiwa katika eneo hilo kwa muda wa miezi mitatu sasa haitavurugwa na kisa hicho.
Ahmed alisema vijana wanne kutoka eneo la Kamologon walivamia kaunti jirani na kufaulu kuiba ng’ombe 30 mnamo jumapili usiku.
“Kufikia hadi sasa tumefaulu kupata na kurejesha ng’ombe saba na tunaahidi tutafanya lolote kuhakikisha kwamba ng’ombe wote wamerudishiwa wenyewe,” mkuu huyo alisema.
Aliendelea kusema kwamba tayari wamepata majina ya vijana wote wanaokisiwa kutekeleza wizi huo na kwamba serikali inafuatilia kuona wamechukuliwa hatua.
Alisema sera ya serikali kwa sasa ni kuwa chifu yeyote lazima arudishe mifugo walioibwa na kupelekwa katika maeneo yao la sivyo watasimamishwa kazi mara moja.
“Hivyo basi natoa onyo kwa machifu wa maeneo ya Marakwet Mashariki wahakikishe ng’ombe hao wamepatikana au wapoteze kazi yao,” Dkt. Ahmed alionya.
Ahmed aliwashukuru viongozi, wawakilishi bunge na wazee kutoka Marakwet kwa juhudi zao kuona amani imedumishwa kwa kuwasaka wanyama hao.
Aliwasihi wenzao kutoka kaunti ya Pokot Magharibi kuongea na vijana kutoka eneo hilo ili kusiwe na visa vyovyote vya kulipisha kisasi wakati viongozi kutoka kaunti ya Elgeyo Marakwet wanawasaka ng’ombe hao.
Alisema visa vya kulipiza kisasa ndivyo husababisha uhasama kati ya jamii hizo mbili jambo ambalo wanajitahidi kuzuia,
Na Alice Wanjiru