Monday, December 23, 2024
Home > Counties > Bungoma > Baraza la magavana laitisha usahihishaji wa sahihi za mchakato wa ripoti ya BBI.

Baraza la magavana laitisha usahihishaji wa sahihi za mchakato wa ripoti ya BBI.

Mwenyekiti wa Baraza la magavana nchini Wycliffe Oparanya ameitaka tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC kuharakisha mchakato wa kuhakikisha usahihi wa saini zilizowasilishwa mbele yake ili kufanikisha kufanyika kura ya maamuzi.

          Akizungumza alipohudhuria ibada ya Jumapili katika kanisa katoliki la Christ the King mjini Bungoma, Oparanya alisema Tume hiyo imechukua muda mrefu sana kusahihisha saini hizo.

            “Tunaiambia tume ya IEBC iharakishe kusahihisha saini hizo kwa sababu sisi tuko tayari kuipigia kura,” alisema Gavana Oparanya.

Kwa upande wake gavana wa jimbo la Bungoma, Wycliffe Wangamati aliwataka wakazi kuisoma ripoti ya BBI ili kufahamu yaliyomo kabla ya kutoa uamuzi wa kuunga mkono msuada wa marekebisho ya katiba wa 2020.

“Mimi nawaomba wapinzani wangu tushirikiane pamoja ili tuwafanyie watu wetu maendeleo,” Wangamati kasema.

             “Sisi kama watu wa Bungoma inafaa tukae chini na tujiulize ni nini kizuri kilichomo katika ripoti hiyo ya BBI ili tufanye uamuzi wetu wa kuiunga mkono ama kuikataa,” alisema Gavana Wangamati.

          Waziri wa Ugatuzi Eugene Wamalwa ambaye pia alihudhuria hafla hiyo alitoa wito kwa viongozi wa kisiasa kusitisha siasa ili kuziruhusu serikali za kaunti na ile ya kitaifa kutekeleza miradi ya maendeleo katika kipindi kilichosalia.

“Tafadhali wanasiasa mwaka huu sio wa siasa kwa hivyo tuweke kando masuala ya kisiasa na tuwafanyie wakenya maendeleo,” alikariri waziri Wamalwa.

Na Roseland Lumwamu

Leave a Reply