Watu kumi na watatu waliokuwa katika karantini nyumbani mwao katika eneo la Rongai, Nakuru, sasa wameachiliwa kutangamana na wengine baada ya majibu yao kuthibitisha kuwa hawana virusi vya korona.
Kwa mujibu wa naibu kamishna wa eneo hili Ronald Mwiwawi, kumi na watatu hawa waliotoka katika nchi tofauti tofauti za ng’ambo, walimaliza muda wao wa siku 14 za karantini kama inavyopendekezwa lakini waliona vyema kuwaongezea siku saba zaidi za kujikarantini baada ya gatuzi la Nakuru kupata wagonjwa wawili waliokuwa na virusi vya covid-19.
Mwiwawi aliendelea kusema kuwa hata iwapo wameachiliwa, kuna umuhimu wa kuendelea kuzingatia masharti yaliyotolewa na serikali kwani janga hili bado lipo na iwapo watazembea basi wataambukizwa virusi hivi.
Hata hivyo, Mwiwawi alidokeza kuwa watu hawa wamepata ushauri nasaha utakao wawezesha kuyaendeleza maisha yao shwari bila wasiwasi wowote.
Aidha, aliziomba familia zao kuwakubali kikamilifu kwa kuwaonyesha upendo akiongezea kuwa jamii ina jukumu la kuhakikisha kuwa wale wote wanaotoka katika karantini wakiwa salama pamoja na wale wanaopona kutokana na virusi vya covid-19 hawakumbwi na unyanyapaa bali wapate msaada mwafaka kuwawezesha kuendelea na maisha yao kama awali.
Kumi na watatu hawa wamekuwa wakitembelewa na maafisa wa afya walipokuwa katika karantini ili kuhakikisha kuwa masharti yanazingatiwa kikamilifu.
Na Emily Kadzo