Friday, December 27, 2024
Home > Counties > Wenyeji wahimizwa kupata chanjo ya Korona

Wenyeji wahimizwa kupata chanjo ya Korona

Idara ya Afya katika kaunti ya Kakamega imewahimiza wakazi wa gatuzi hilo kupata chanjo ya Korona ili kujikinga dhidi ya makali ya ugonjwa huo hatari.

Akitoa wito huo, Afisa wa uhamasishaji wa Afya katika Kaunti hiyo Bi Tabitha Kiberenge amewahakikishia wakazi wa gatuzi hilo kuwa chanjo hiyo imefanyiwa majaribio na kuthibitishwa kuwa salama.

“Chanjo ni njia moja ya kuweza kuzuia janga, na lengo letu ni kwamba angalau asilimia 70 ya wakazi wa Kakamega wapate chanjo ya Korona,” alisisitiza Kiberenge.

Alisema awali Kakamega ilikuwa nambari ya tatu kwenye orodha za kaunti hapo awali kwa kuchanja watu dhidi ya korona lakini sasa imeshuka hadi nafasi ya tano katika Kenya nzima.

“Tusipofanya jambo tutaendelea kurudi nyuma,” alisisitiza akionya kuwa maambukizi yanaendelea kushuhudiwa kila siku.

Aliwashauri kupuuza mila na itikadi ambazo ni  baadhi ya vizuizi kwa wakazi kupata chanjo hiyo  ya Korona.

Afisa huyo alikuwa akizungumza katika mkutano  wa uhamasisho uliojumuisha mashabiki wa Timu ya Kandanda ya Kakamega Homeboyz, AFC Leopards, Mashabiki wa Arsenali,Viongozi wa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu na Vyuo Anuwai na Vikundi vya Maonyesho ya Kuigiza.

Kiberenge alisikitika kuwa wakazi wengi wanapuuza maagizo yaliyotolewa na Wizara ya Afya ya kuzuia msambao wa ugonjwa huo wa Korona.

Alisema ugonjwa wa Korona bado upo akiwahimiza kuendelea kutumia barakoa, kuzingatia umbali wa mita moja na kunawa mikono ili kuepuka kuambukizana ugonjwa huo.

Akizungumza katika kikao hicho, Kamanda wa Mashabiki wa timu ya Kakamega Homeboyz, Collins Lumumba, alisema walikuwa wanapuuza maagizo wakidhani ugonjwa wa korona umeisha.

Aliwasihi maafisa wa Afya kuzuru uwanja wa mpira wa Bukhungu ili kuwapa chanjo mashabiki tarehe 24 mwezi huu wakati timu ya Kakamega Homeboyz itakuwa ikimenyana na AFC Leopards.

Na Rose Adelaide

Leave a Reply