Monday, December 23, 2024
Home > Counties > Miili minne haijatambuliwa katika hospitali ya Iten

Miili minne haijatambuliwa katika hospitali ya Iten

Mwanakamati kuu (County Executive Committee) anayesimamia afya katika kaunti ya Elgeyo Marakwet Kiprono Chepkok amewataka wananchi ambao wamepoteza watu wao wafike katika hospitali ya Iten kuona kama wamo miongoni mwa miili minne ambayo imekuwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali hiyo.

Chepkok alisema kwamba miili hiyo imesalia katika chumba hicho kwa muda wa kati ya miezi sita hadi mwaka mmoja akiongeza kwamba wananuia kwenda mahakamani kutafuta amri ya kuizika.

Akizungumza na wanahabari afisini mwake mjini Iten, Chepkok alisema hospitali hiyo haitawatatoza ada yoyote wakija kuchukua miili hiyo.

Alisema moja ya maiti hiyo ililetwa na polisi baada ya kuuawa katika kisa cha wizi wa mifugo katika mipaka ya kaunti ya Elgeyo Marakwet na Baringo huku mwingine mwenye asili ya kiganda akiaga baada ya kulazwa hospitalini humo.

“Shida kubwa tulionayo ni kuwa watu hawa hawakuwa na stakabadhi zozote ambazo zinaweza kuwatambulisha na hivyo inakuwa vigumu kwetu kuwatafuta jamaa wao,” alisema Chepkok.

Mwanakamati huyo alisema kaunti hiyo hutumia pesa nyingi kusafirisha maiti hadi kaunti jirani ya Uasin Gishu kwani hakuna makaburi ya umma katika kaunti hiyo.

“Tunatakiwa kugharamia usafirishaji, kununua jeneza, pahali pa kuzika na hata kuwalipa watakaochimba kaburi,” alisema Chepkok.

Mwanakamati huyo alisema kuna haja ya kuwa na makaburi ya umma katika kaunti akisema hili litaokoa fedha ambazo kaunti hutumia visa kama hivi vinapotokea.

Wakazi katika kaunti wamedinda kuiuzia kaunti ardhi itakayotengewa makaburi wakisema ya kwamba ni mwiko kuishi karibu na makaburi ya umma.

Hata hivyo Chepkok anasema kaunti inaendelea kukua na kuwavutia watu kutoka sehemu mbali mbali ambao watahitaji huduma za makaburi ya umma.

Alisema katika mpango shirikishi wa maendeleo katika kaunti, kaunti hiyo inanuia kuwa na makaburi ya umma katika kila kaunti ndogo ijapokuwa changamoto kuu ni kupata ardhi.

By Alice Wanjiru

Leave a Reply