Friday, November 22, 2024
Home > Counties > Wazazi Kilifi walilia msaada kupeleka watoto wao shuleni

Wazazi Kilifi walilia msaada kupeleka watoto wao shuleni

Wazazi kutoka Kaunti ya Kilifi, wanaililia serikali na mashirika ya kufadhili wanafunzi kujitokeza na kusaidia watoto wao ambao kufikia sasa wameshindwa kujiunga na shule za upili, kwa sababu ya ukosefu wa karo.

Kundi la wazazi kutoka kijiji cha Jimba Mjini Watamu, walielezea wanahabari kwamba watoto wao waliopata alama kati ya 250 na 340, hawajaweza kupata msaada wowote kutoka kwa serikali na mashirika ya ufadhili hali ambayo imeacha watoto wengi wakisalia majumbani bila matumaini ya kwenda shuleni kwani wazazi hao hawana uwezo.

Kufikia sasa, zaidi ya wanafunzi 17 kutoka kijiji hicho hawajaweza kuripoti shuleni, huku wazazi wakitapatapa wasijue hatima ya watoto wao.

Tangu shule zifunguliwe, Mzee Omari Juma amekuwa na msongo wa mawazo mengi.  Binti yake mwenye ndoto ya kuwa mhudumu wa ndege alifuzu kwa alama 327 na kuitwa shule ya wasichana ya Ngala. Ana hamu kubwa ya kuendelea kimasomo lakini amekosa uwezo wa kumpeleka shule ya upili.

Juma anaeleza kuwa alipoteza kazi yake ya upishi hotelini wakati wa janga la Covid-19 hali iliyomuweka chini kiuchumi. Sasa hajui afanye nini kwani amezunguka kila ofisi kutafuta msaada bila mafanikio. Binti yake, anamlilia kwa machozi kila siku lakini asijue la kumwambia.

Juma alilalamika kwamba mashirika mengi ya ufadhili yanayojitokeza kusaidia, huchagua watoto waliopata alama 350 na zaidi hivyo kuacha watoto wengi wenye uhitaji wa usaidizi wa karo kukata tamaa ya kuendelea na masomo.

“Msichana wangu alipata alama ya 327, na wengi wanaofadhiliwa ni wale wa kuanzia 350. Alikua na uwezo wa kupata hizo na aling’ang’ana lakini hakuweza. Ombi langu ni kwamba wale ambao walipata alama chini ya hizo wapate misaada pia kwa sababu ni wanafunzi ambao wanapenda kusoma vile vile,” alisema.

“Nimejaribu kung’ang’ana lakini nikashindwa kabisa. Nimejaribu kutembelea kila mahali ili nipate usaidizi lakini nimeshindwa kabisa mpaka sasa msichana wangu kila nikiamka asubuhi huwa nasikitika kwa sababu huwa analia machozi anasema baba nitapelekwa shule lini mimi,” alieleza kwa masikitiko.

Hali sio tofauti kwa Mzee Pole Kai kutoka kijiji cha Gede. Mwanawe alipata alama ya 315, na kuitwa shule ya upili ya Ngala lakini juhudi za kutafuta pesa na misaada mbali mbali zimeambulia patupu. Hali hii imemlazimu bintiye kubaki nyumbani wenzake wakianza masomo.

Kai ameomba mashirika yanayotoa misaada waweze kujitokeza kusaidia watoto ambao walipata alama za wastani ili pia wapate fursa ya kujiunga na shule za upili.

Mzee wa mtaa eneo hilo ambaye pia ni mchungaji Bwana Eliud Kazungu alisema kwamba vijana wengi waliopata alama zaidi ya 250, wamebaki mtaani hali inayowaweka katika hatari ya kujiingiza kwenye uhalifu hivyo akasisitiza kwamba kuna haja ya mashirika kuongeza usaidizi ili kufikia wanafunzi wote ambao walipata alama zinazoridhisha ili waweze kuenda shuleni.

“Hawa watu walipata maksi nzuri, walifikisha hadi 340 lakini hawakuweza kusaidiwa kwa sababu anaangaliwa wa alama 350. Ningeomba kama mwananchi kwamba tushirikiane ili tusaidie kutoka angalau 250 na kuendelea. Hio tutasaidia watu wengi watakaosaidia Kenya katika siku za usoni,” alisema.

Wasichana watatu walioathirika na ukosefu huo wa karo waliandamana na wazazi wao walipotembelewa na wanahabari na kuelezea masikitiko makubwa na hofu kwamba ndoto zao za maisha huenda zikadidimia.

Watoto hao walio chini ya umri wa miaka 17, wameomba msaada ili waweze kuendelea na masomo na kuepuka matatizo yanayowakodolea macho kama vile mimba za mapema.

Mamia ya watoto ndani ya Kaunti ya Kilifi, wanahofiwa kukwama majumbani kwa sababu ya ukosefu wa fedha za kugharamia karo na mahitaji mengine shuleni, huku wanafunzi walioathirika zaidi wakiwa watoto waliopata alama za wastani hadi alama 340.

Na Jackson Msanzu

Leave a Reply