Friday, November 22, 2024
Home > Counties > Bungoma > Gereza la Bungoma lapata msaada wa vipakatarakilishi kurahisisha kesi

Gereza la Bungoma lapata msaada wa vipakatarakilishi kurahisisha kesi

Kufuatia kuzuka kwa janga la Covid-19 nchini, sekta mbalimbali ziliathirika na nyingi za shughuli zikalazimika kusitishwa kwa muda.

Katika idara ya mahakama, mfumo wa kutumika kwa kusikiza kesi za wafungwa ulibadilika na mfumo wa teknolojia ukakumbatiwa.

Idadi ya watu iliyohitajika kufika kortini kusikiza ama kuhudhuria kusikizwa kwa kesi zao ilipunguzwa na baadae ikalazimika kesi nyingi kufanywa kupitia njia ya mtandaoni ili kuzuia msambao wa virusi vya Corona kutoka kwa mtu mmoja hadi mwengine.

Hali hiyo iliweza kuwa changamoto si haba kwa idara ya mahakama na idara ya magereza katika kaunti ya Bungoma ambapo hazikuwa zimejipanga vilivyo kwa kuwa na vipakatalishi vya kutosha vya kusaidia kuendeleza shughuli zake za kesi kupitia mitandaoni na hivyo iliweza kusababisha kesi nyingi za watu kufanywa kwa kujikokota na kuchukua muda mrefu kabla ya kutamatika.

Kufuatia hali hiyo idara ya mawakili tawi la Bungoma, kwa ushirikiano na idara ya mahakama ya Bungoma, ziliweza kununua vipakatalishi viwili na kupeana kwa idara ya magereza ya Bungoma ili kusaidia kesi za watu ziweze kufanywa kwa wakati ufaao.

Akizungumza baada ya kupokezwa vifaa hivyo msimamizi mkuu wa Gereza la Bungoma, Hassan Mukavani,alifichua kuwa awali walikuwa na vipakatarakilishi viwili  ambapo ilikuwa vigumu kwao kufanya kesi Kwa haraka.

“Hapo awali tulikuwa na vipakatarakilishi viwili pekee ambavyo vimekuwa vikihudumia koti nane zilizomo katika kaunti hii ambapo imekuwa vigumu koti hizi kuendeleza shughuli zake Kwa wakati mmoja,

“Wakati mwingine koti moja inamaliza kushughulikia kesi ndio waunganishe kwa nyingine ili iendeleze shughuli zake na hivyo kufanya kazi kuwa ngumu kwa sababu tunafanya kazi hadi saa kumi na mbili jioni”, alisema Bw. Hassan.

Mahakama hizo ni pamoja na Bungoma,Webuye,Sirisia na Kimilili.

Hata hivyo, Mukavani alitoa changamoto kwa wahisani mbalimbali kujitokeza na kuwaongezea vipakatarakilishi vingine ili kuhakikisha kuwa kazi yao inarahisishwa.

“Tumeshukuru sana kwa kupewa vyombo hivi lakini bado tunahitaji zaidi ili kurahisisha wafungwa kuzikizwa kwa haraka ili mambo yao yaende vizuri”, alisema Bw. Hassan.

Akizungumza, Mwenyekiti Wa Mawakili tawi la Bungoma,Benjamin Osiula, alisema kutokana na uhaba wa vipakatarakilishi uliokuwa ukishuhudiwa na kusababisha wateja wao kuhangaika ndipo ikawapa msukumo wa kununua kompyuta  zaidi ili kuongezea kwa idadi iliopo ili kuwapunguzia madhila wateja wao.

“Sisi wenyewe kama wachezaji katika uwanja huu, wateja wetu wanaumia ndiposa tukasema iwapo idara ya mahakama itaweza kupata kompyuta, nasi pia mawakili tuongezee ingekuwa vizuri ili kupunguza kazi wakati mahakama ya juu inapofanya kesi za wale walio ndani mle magerezani, pia hizi mahakama za chini ziweze kuendelea ili kesi za watu zikamilike kwa wakati ufaao maanake watu walio gerezani wanastahili kupata haki kama wale walio nje kwa dhamana,”alieleza Osiula.

Na Dishon Amanya

Leave a Reply