Friday, November 22, 2024
Home > Counties > Wachongaji sanamu walia ngoa kwa kukosa soko Malindi 

Wachongaji sanamu walia ngoa kwa kukosa soko Malindi 

Wachongaji wa vinyago mjini Malindi wanalalamikia kutopata soko la bidhaa zao kufuatia chimbuko la ugonjwa hatari wa korona nchini.

Wasanii hao, ambao ni wanachama wa Malindi Handcraft Cooperative Society, wamesema kuwa miaka ya nyuma walikuwa wakipata zaidi ya shilingi milioni 37 kila mwaka ila tangu janga la korona kuripotiwa nchini, sasa wanapata chini ya shilingi laki moja pekee.

Wanachama hao wanaotekeleza taaluma ya uchongaji vinyago katika eneo la Muyeye, mjini Malindi wameziomba sikerikali kuu na ile ya kaunti ya kilifi kuwatafutia soko na wafadhili ambao watapanua soko lao la vinyago.

Akiongea na waandishi wa habari katika karakana ya sanamu huyo Muyeye mjini Malindi Ijumaa, Mwenyekiti wa chama hicho cha ushirika, Bw. Cosmas Kyalo, pia alisikitika kuwa biashara yao haijafaidika na ufadhili wa fedha zilizotolewa ili kufufua biashara za utalii katika sehemu hiyo.

“Shida kubwa ni ukosefu wa soko. Tangu mwaka jana tulipokumbwa na janga hili, hatujapata msaada wowote kutoka kwa serikali. Naiomba serikali itupatie msaada,” Cosmas alisema.

John Nzao, ambaye alisema ametegemea uchongaji wa vinyago kwa miaka mingi, alikiri ya kwamba wafanyikazi wengi kwenye karakana hiyo wamekosa pesa za kujikimu kimaisha kutokana na upungufu wa mauzo.

“Tulikuwa wafanyikazi 600 lakini sasa  tumebaki sabini pekee. Wengi  wamerudi vijijini kutafuta ajira nyingine ili  waweze kukidhi mahitaji ya familia zao,”  Nzao alisema.

Kiwanda hicho huchonga vinyago vinavyowavutia sana watalii, mbali na kupata wateja hapa nchini, wameweza kusafirisha michongo yao katika nchi za ng’ambo ila siku hizi mambo yamebadilika.

Eneo la Malindi limekuwa kivutio cha watalii kwa muda kutokana na mandhari yake na makavazi yanayohifadhi historia za jamii mbalimbali.

na Emmanuel Masha 

 

Leave a Reply