Friday, November 22, 2024
Home > Counties > Bungoma > Magavana nchini wawaambia wahudumu wa afya wanaogoma wasahau kulipwa

Magavana nchini wawaambia wahudumu wa afya wanaogoma wasahau kulipwa

Huku wahudumu wa afya wakiendelea na mgomo wao, magavana nchini wanaendelea kuwasuta vikali kwa kulemaza sekta ya afya na kuwaacha wakenya wa kawaida wakitaabika kwa kukosa huduma.

            Akizungumza wakati alipohudhuria ibada ya Jumapili katika kanisa la Reformed East Africa mjini Bungoma, gavana wa Uasin Gishu Jackson Mandago aliwataka wahudumu wa afya kusitisha mgomo wao na kurudi kazini mara moja, akisema serikali za kaunti hazina pesa za kuwalipa watu wachache.

Gavana Mandago alidokeza kuwa wahudumu wa afya hulipwa vizuri na serikali za kaunti kuliko wafanyakazi wengine.

            “Wafanyakazi wanaopata mishahara minono katika kaunti zetu ni wahudumu wa afya sioni haja ya wao kugoma. Tunawaambia warudi kazini mara moja.” alisema gavana Mandago.

            Alisema kuwa kazi ya huduma ya afya ni mwito huku akiwataka wahudumu wa afya kujitolea na kuwahudumia wananchi wala sio kuweka mbele maslahi yao ya kibinafsi.

            “Kazi ya huduma ya afya ni mwito na kama hauna mwito tafuta kazi nyingine ya kufanya,” alieleza Mandago.

Yanajiri hayo, wahudumu wa afya wakishikilia msimamo wao kuwa  hawatarejea kazini hadi pale matakwa yao yatakaposhughulikiwa ipasavyo.

Mahitaji hayo ni miongoni mwa; kupewa bima ya afya, NHIF, kupewa mavazi ya kujikinga na virusi vya Covid-19.

            Kwa upande wao, viongozi wa kanisa hilo la Reformed East Africa walilitaka Baraza la Magavana nchini kusikia kilio cha wahudumu wa afya wanaogoma na kuwatekelezea mahitaji yao, wakitaja kwa sasa wakenya wa kawaida wanaumia kwa kukosa huduma muhimu za afya.

           Wakiongozwa na Kasisi Barasa Wanyonyi, walisema kuwa Baraza la Magavana kukawia kusuluhisha mgomo huo, huenda wakenya wengi wakapoteza maisha yao hivi karibuni kwa kukosa matibabu.

 

na Roseland Lumwamu

Leave a Reply