Shirika la Msalaba Mwekundu limefadhili ujenzi wa chumba kitakachotumiwa kupima ugonjwa wa Corona katika jela ya Tambach kaunti ya Elgeyo Marakwet kilichogharimu Sh300, 000.
Mweka hazina wa shirika hilo katika kaunti hiyo Dickson Kimutai alisema kando na ujenzi, wamenunua vifaa vitakavyotumika kama vile kifaa cha kupima joto,vifaa vya kuosha mikono na pia vitakasio.
Akizungumza katika jela hiyo, Kimutai alisema walichukua hatua hiyo kama mchango wao wa kuhakikisha kwamba kila mwananchi anapata kinga dhidi ya kuambukizwa virusi vya corona.
“Wafungwa na wanaowekwa rumande huletwa mara kwa mara na kwa hivyo ni muhimu kuhakikisha kuwa jela ni mahali ambapo panakingwa kutokana na ugonjwa huu ambao umeenea duniani kote,” alisema Kimutai.
Afisa anayesimamia jela hiyo Francis Itulia alisema chumba hicho kitasaidia pakubwa katika kupigana na vita dhidi ya kusambaa kwa virusi vya corona akisema kwa sasa wana uwezo wa kuwahudumia wafungwa 100 kwa siku.
Alisema mfungwa yeyote atakayepatikana na dalili za corona ataweza kuhudumiwa katika hospitali ya Tambach.
Gavana wa Marakwet Alex Tolgos amewataka wakaazi kuendelea kuzingatia hatua zilizowekwa na serikali kupigana na janga la corona akisema wengi wanaendelea kuzipuuza ilhali ugonjwa huo bado ni tisho kwa wanadamu.
Tolgos alizitaka kaunti jirani kama vile Baringo kushughulikia matakwa ya wahudumu wa afya akisema kaunti ya Elgeyo Marakwet imekuwa ikibeba mzigo mzito kuwahudumia wagonjwa kutoka kaunti hiyo baada ya wahudumu wao kugoma.
Alionya kuwa hali hiyo ikiendelea basi kaunti hiyo itakosa dawa na vifaa vingine vya kuwahudumia wagonjwa.
Na Alice Wanjiru