Saturday, November 23, 2024
Home > Counties > Bungoma > Hofu ya kuzuka kwa ugonjwa wa kipindupindu Mlima Elgon

Hofu ya kuzuka kwa ugonjwa wa kipindupindu Mlima Elgon

Huenda wakaazi wa Cheptais katika eneo bunge la Mlima Elgon wakapata maradhi ya kipindupindu kutokana na ukosefu wa maji safi katika eneo hilo.

Kulingana na msimamizi mkuu wa maabara katika kituo cha afya cha Cheptais Fredrick Ndiema, ipo haja idara husika kuchukua hatua ya haraka ya kulinda mazingira na chemchemi za maji katika Mlima Elgon ili kudhibiti mkurupuko wa ugonjwa wa kipindupindu ambao huenda ukazuka wakati wowote.
Ndiema pia ametoa wito kwa wahisani pamoja na serikali ya kaunti kutoa msaada wa vifaa vya matibabu kwa hospitali hiyo ili kuhakikisha kuwa wagonjwa wanaotafuta tiba eneo hilo wanasaidika pakubwa.
Usemi huo unarejelea kilio cha wakazi wa eneo hilo ambao wanalalamikia barabara mbovu, maji chafu pamoja na ukosefu wa vituo vya afya katika eneo hilo la Mlima Elgon, jambo ambalo wanasema limekuwa kero kwao huku wakizitaka idara husika kuingilia kati na kuwasaidia.
Akitoa msaada wa mitungi ya maji ya lita mia moja kwa hospitali ya Cheptais,Mwenyekiti wa klabu ya Rotary eneo la Magharibi, Peter Mudanya, amesisitiza haja ya ushirikiano kati ya serikali ya kaunti pamoja na wadau mbalimbali ili kuwaokoa wakazi wa Mlima Elgon kutokana na changamoto wanazopitia.

Na Roseland Lumwamu

Leave a Reply