Monday, December 23, 2024
Home > Counties > Waislamu wanaiomba serikali kufungua misikiti wakati wa Mwezi wa Ramadhan

Waislamu wanaiomba serikali kufungua misikiti wakati wa Mwezi wa Ramadhan

Viongozi wa Kiislamu katika kaunti ya Mombasa wameiomba serikali kuruhusu kufunguliwa kwa misikiti wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhan unaoanza wiki ijayo.
Viongozi hao wakiwemo maimamu na wabunge pia wameisihi serikali kupunguza masaa ya kutotoka nje wakati wa mwezi wa Ramadhan kuanzia saa nne usiku hadi saa kumi na moja alfajiri ili kuwawezesha waumini wa kiislamu kutekeleza ibada wakati wa jioni.
Wakihutubia waandishi wa habari katika ukumbi wa Baluchi, viongozi hao chini ya baraza la maimamu humu nchini (CIPK) waliahidi kuwa watahakikisha masharti yote yaliyowekwa na Wizara ya Afya yatatekelezwa iwapo ombi lao litakubaliwa.
“Tutahakikisha usafi wa kunawa mikono na kutokaribiana wakati wa maombi utafuatwa kikamilifu,” alisema Katibu Mtendaji wa Baraza la Maimamu Sheikh Mohamed Khalifa.
Sheikh Khalifa alisema mwezi mtukufu wa Ramadhan ni ibada muhimu kwa waislamu ambayo ni nguzo ya nne miongoni mwa nguzo tano za dini ya kiislamu.
Alisema waislamu watatumia fursa hiyo kumuomba Mungu awanusuru wakenya na ulimwengu wote kwa jumla janga la virusi ya Corona.
Sheikh Khalifa alisema wanaunga mkono juhudi za serikali za kuzuia kuenea kwa maradhi hayo ambayo yameleta hangaiko ulimwengu mzima na kusababisha vifo katika mataifa kadhaa.
Wakati huo huo, Sheikh Khalifa aliiomba serikali kutoa msaada wa chakula kwa waislamu wasiojiweza wakati wa mwezi wa Ramadhan.
Alisema ni muhimu kwa serikali kuwasaidia waislamu walio na mapato ya chini na ambao wameathirika pakubwa na janga la Corona.
Seneta wa Mombasa Mohamed Faki na Mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir ambao walikuwako wakati wa mkutano huo waliunga mkono maombi hayo ya viongozi wa kiislamu.

Na Mohamed Hassan

Leave a Reply